Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 RUANGWA YATAKA ELIMU ENDELEVU KUHUSU SHERIKA ZA KAZI SEKTA YA MADINI KWA WAAJIRI NA WAAJIRIWA

RUANGWA YATAKA ELIMU ENDELEVU KUHUSU SHERIKA ZA KAZI SEKTA YA MADINI KWA WAAJIRI NA WAAJIRIWA

 

NA HADIJA OMARY 

RUANGWA – Serikali Wilayani Ruangwa, Mkoani Lindi, imeitaka Ofisi ya Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Lindi kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuandaa mpango mahususi wa kuendelea kutoa elimu kuhusu sheria, taratibu, wajibu na haki katika sekta ya madini kwa waajiri na waajiriwa.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Zuhura Omary, alipokuwa akizungumza na waajiri wa sekta binafsi wakati wa mafunzo kuhusu Sheria za Kazi na mabadiliko yake yaliyofanyika wilayani humo.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Ofisi ya Afisa Kazi Mfawidhi Mkoa wa Lindi kwa kushirikiana na NSSF, kwa lengo la kuimarisha uelewa wa sheria za kazi na kupunguza migogoro mahali pa kazi.

Mhandisi Zuhura alisema serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi kama chanzo kikuu cha ajira, akitaja kuwa sekta ya madini pekee Wilayani Ruangwa inaajiri kundi kubwa la wananchi. 

Kwa upande wake, Afisa Kazi Mfawidhi kutoka Idara ya Kazi na Ajira, Nisetas Bureta, alieleza kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa kuwajengea uelewa waajiri kuhusu sheria za kazi na mabadiliko yake ya hivi karibuni.

Naye Meneja wa NSSF Mkoa wa Lindi alitumia fursa hiyo kutoa tahadhari kwa wanachama wanaofuatilia mafao yao, kuwataka kujiepusha na matapeli wanaojitambulisha kuwa maajenti wa mfuko huo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na tija na wakaomba elimu kama hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko ya sheria na mazingira ya kazi.

MWISHO

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3