PATUTA ORGANIZATION, MACHIFU WANOGESHA SIKU YA UTAMADUNI DUNIANI VISIWANI ZANZIBAR
Na. Mwandishi wa Matukio Daima Media, Zanzibar.
UNGUJA, Mei 22, 2026 Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA Organization) na Machifu kutoka maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara na Taifa la Afrika Kusini wamepamba usiku wa kilele cha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Utamaduni Duniani yanayoandaliwa na Tume ya Taifa ya UNESCO (UNESCO NATCOM) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dr. Aiden Ndaombwa ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa PATUTA amesema tamasha hilo limeleta chachu kwa taasisi anayoiongoza ambayo inashirikiana na Machifu katika kulinda na kutunza mila na desturi za mwafrika ambapo Tanzania na Zanzibar zinajivunia kulinda tamaduni hizo kwa muda mrefu sasa.*
"PATUTA Organization tunajisikia furaha kuwa miongoni mwa washiriki wakubwa katika tamasha hili la utamaduni na wenzetu wa UNESCO NATCOM, Machifu kutoka sehemu mbalimbali wameweza kutembelea vivutio vya Utalii lakini pia kujionea shughuli za utamaduni zinazofanywa na jamii ya Visiwani Zanzibar." Amesema Dkt.Aiden Ndaombwa.
Tamasha hilo shamrashamra zake zilianza Mei 19 na kilele chake usiku Mei 21, 2026 likiwa na lengo la kusherehekea utofauti wa kitamaduni duniani (Cultural Diversity) na kukuza maelewano baina ya jamii mbalimbali.
Aidha, vikundi mbalimbali vya Ngoma na Wasanii wameweza kutoa burudani na maonesho na michezo ya asili na utamaduni imeweza kuoneshwa sambamba na mjadala maalum juu ya utekelezaji wa mikataba ya kitamaduni ya UNESCO.
Mwisho.






