MDEMU AWATAKA WANAWAKE KUTUMIA VEMA VIKUNDI VYA KIUCHUMI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amewataka wanawake nchini kutumia vikundi vya kiuchumi kama nyenzo ya kujikwamua kiuchumi huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha heshima, upendo na mshikamano ndani ya familia zao.
Akizungumza Mei 11, 2026 katika kijiji cha Kipaduka, kata ya Uhambingeto wilayani Kilolo mkoani Iringa, wakati wa mafunzo ya muongozo wa uanzishwaji na uwezeshaji wa majukwaa ya wanawake kiuchumi, Mdemu alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya jamii.
Alisema majukwaa ya wanawake yamekuwa daraja muhimu la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia ushirikiano, mikopo midogo, mafunzo ya ujasiriamali pamoja na kubadilishana uzoefu wa kimaendeleo, jambo ambalo limeanza kuleta matokeo chanya katika maeneo mbalimbali nchini.
“Wanawake wanapaswa kutumia fursa za vikundi kujenga uchumi wao, kuongeza kipato cha familia na kujiletea maendeleo. Lakini pamoja na mafanikio hayo, ni muhimu kuendelea kuthamini nafasi ya familia na kuheshimu waume zenu ili kuendelea kujenga jamii yenye amani na mshikamano,” alisema Mdemu.
Aidha, alisema Serikali kupitia wizara hiyo itaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wanawake ili kuhakikisha wanapata maarifa sahihi ya uongozi, usimamizi wa fedha na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa tija.
Mdemu alibainisha kuwa wanawake wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii katika vikundi mbalimbali, lakini changamoto ya ukosefu wa elimu ya usimamizi wa miradi na matumizi sahihi ya fedha bado ipo, hali inayochangia baadhi ya vikundi kushindwa kudumu kwa muda mrefu.
Alisisitiza umuhimu wa wanawake kushirikiana ndani ya vikundi vyao kwa uwazi na uaminifu ili kuepusha migogoro inayoweza kudhoofisha malengo ya maendeleo waliyojiwekea.
Kwa upande wao, baadhi ya wanawake walioshiriki mafunzo hayo waliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapatia elimu inayowajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi huku wakiahidi kutumia mafunzo hayo kuboresha shughuli zao za uzalishaji mali.
Mwenyekiti wa jukwaa hilo alisema wanawake wa kata ya Uhambingeto wamejipanga kutumia fursa za majukwaa hayo kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo na biashara ndogondogo ili kuongeza kipato cha kaya zao.
TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII
Mafunzo hayo ya muongozo wa uanzishwaji na uwezeshaji wa majukwaa ya wanawake kiuchumi yamelenga kuwajengea wanawake uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi katika ngazi ya jamii.
















