MCC ASAS NA MCC ABOOD WAUNGANA KUOMBA KURA ZA MTATIFIKOLO UBUNGE ISIMANI
Na Matukio Daima Media Isimani.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Salim Asas ameahidi kumpa ushirikiano mkubwa mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani kupitia CCM, Emanuela Mtatifikolo katika kuhakikisha anapata ushindi mkubwa na kuendeleza maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Asas alitoa kauli hiyo leo Itunundu Pawaga wakati alipoungana na Mohamed Abood ambaye pia ni mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa katika shughuli ya kumnadi Mtatifikolo mbele ya wananchi wa Isimani.
Katika mkutano huo viongozi hao walieleza imani yao kubwa kwa mgombea huyo wakisema ana uwezo mkubwa wa kuwatumikia wananchi kutokana na uzoefu wake wa kazi na ushirikiano aliouonyesha kwa muda mrefu ndani ya chama.
Akizungumza mbele ya wananchi na wanachama wa CCM, Asas alisema kuwa kama mdau mkubwa wa maendeleo katika Mkoa wa Iringa na hasa Jimbo la Isimani, amekuwa akitoa ushirikiano wa karibu kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu William Lukuvi na kwamba ataendelea kufanya hivyo kwa Mtatifikolo ili kuhakikisha maendeleo yaliyopo yanaendelea kusonga mbele.
Alisema anamfahamu vizuri Mtatifikolo kutokana na kufanya naye kazi kwa kipindi kirefu na hivyo anaamini wananchi wa Isimani watanufaika na uchapakazi wake pamoja na uwezo wake wa kusimamia maendeleo ya wananchi.
“Namfahamu sana Mtatifikolo, ni mchapakazi mkubwa na nimefanya naye kazi kwa muda mrefu. Nina imani wananchi wa Isimani watanufaika sana na uwezo wake wa kufanya kazi pamoja na kusimamia maendeleo ya jimbo hili,” alisema Asas.
Kwa upande wake, Abood aliwataka wananchi wa Isimani kujitokeza kwa wingi wakati wa uchaguzi ili kumpa kura nyingi mgombea huyo wa CCM. Alisema chama kina imani kubwa kwa Mtatifikolo na kinaamini atakuwa kiongozi bora atakayesimamia maendeleo ya wananchi pamoja na kuendeleza miradi iliyoanzishwa katika jimbo hilo.
Aidha, Abood alisema mshikamano ndani ya CCM ni mkubwa na kwamba viongozi pamoja na wanachama wameamua kuungana kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, waliokuwa watia nia wa nafasi ya ubunge ndani ya CCM katika Jimbo la Isimani walitangaza kumuunga mkono rasmi Mtatifikolo.
Waliokuwa watia nia ubunge Isimani wakiongozwa na Arif Abri aliyeshika nafasi ya nne katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama, walisema wamekubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM na wako tayari kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha ushindi mkubwa unapatikana.
Arif Abri alisema kuwa ushindani wa ndani ya chama umeisha na sasa nguvu zote zinaelekezwa katika kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi huo kwa kishindo. Alisisitiza kuwa wao kama watia nia wenza wataendelea kushirikiana na Mtatifikolo katika kampeni na shughuli mbalimbali za kisiasa kwa manufaa ya wananchi wa Isimani.
Naye Mtatifikolo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa CCM pamoja na wananchi wa Isimani kwa imani waliomuonyesha.
Aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, ataendeleza yote yaliyoanzishwa na marehemu Lukuvi sambamba na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo itakayogusa maisha ya wananchi wa Isimani.
Alisema analifahamu vizuri jimbo hilo pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi wake, hivyo atahakikisha anafanya kazi kwa karibu na wananchi ili kutafuta suluhisho la changamoto hizo na kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.
TAZAMA FULL VIDEO BOFYA LINK HII
>



















































































