Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DC MPOGOLO AWATAKA WAZAZI KUSHIRIKI VIKAO SHULENI

DC MPOGOLO AWATAKA WAZAZI KUSHIRIKI VIKAO SHULENI

 


Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kufatilia  maendeleo ya elimu ya watoto wao kwa kuhudhuria vikao vya shuleni  na kushirikiana na walimu kwa ajili kuongeza ufaulu. 


 Akizungumza katika Shule ya Zawadi iliyopo Tabata Wilayani Ilala Dar es Salaam, Mpogolo amesema mafanikio ya mtoto yanategemea ushirikiano wa pande tatu ambazo ni Serikali, wazazi pamoja na jamii, na wanafunzi wenyewe.


Amesema Serikali ina jukumu la kuboresha miundombinu na kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia kupitia walimu, huku wazazi na jamii wakipaswa kusimamia malezi na kufuatilia mwenendo wa watoto wao.


"Naomba wazazi kushiriki vikao shuleni sambamba na kushirikiana na Walimu na Wanafunzi ili kuongeza kiwango cha taaluma ili wanafunzi wafaulu kwa wingi shuleni" amesema Mpogolo. 



Mkuu wa Wilaya Edward Mpogolo amesema, wanafunzi wanapaswa kuwa na nidhamu, kuzingatia maadili mema na kuongeza bidii katika masomo yao kila wakati. 


“Tunapozungumzia mafanikio ya mtoto lazima tuzungumzie maeneo matatu makubwa. Serikali ina wajibu wake kupitia walimu, wazazi wana wajibu wao, na wanafunzi nao wanapaswa kuwa na nidhamu na bidii,” amesema.


Aidha, amesema changamoto kubwa inayojitokeza katika shule nyingi za serikali ni mwitikio mdogo wa wazazi wanapoitwa kuhudhuria vikao vya shule, tofauti na ilivyo katika shule binafsi ambapo wazazi wengi hujitokeza kwa wingi kufuatilia maendeleo ya watoto wao.



Mpogolo amesema baadhi ya wazazi huwatuma ndugu, wafanyakazi wa nyumbani au hata madereva wa bodaboda kuhudhuria vikao hivyo kwa niaba yao, jambo ambalo linaathiri mafanikio ya kitaaluma ya mwanafunzi kwa kuwa ushirikiano muhimu kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi haukamiliki.


Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imedhamiria kuimarisha ushiriki wa viongozi katika vikao vya wazazi ili kuongeza hamasa ya kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.


Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya msingi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne, akieleza kuwa jamii inapaswa kujitoa kwa hali na mali kuhakikisha watoto wanapata msingi bora wa elimu kwa maendeleo yao ya baadaye.



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3