WANAUME KUJENGEWA UWEZO WA KUJITAMBUA, NA KUIMARISHA FAMILIA ZAO.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Kongamano maalum la wanaume linalotarajiwa kufanyika Jijini Mwanza likiwa na lengo la kuwakutanisha wanaume na kuwapatia elimu ya kujitambua, kujifahamu na kuelewa wajibu wao katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Tukio hilo litakalofanyika Aprilini 26. 2026 linaambatana na maadhimisho ya miaka 11 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Men at Work, Global ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawajengea uwezo wanaume nchini, huku lengo kuu ni kumwezesha mwanaume kuboresha maisha yake na ya wale wanaomzunguka.
Akizungumza na Waandishi wa Habari rais na Mwanzilishi wa taasisi ya wanaume Tanzania (Men at Work Global) Maxwell Shing'oma ameeleza kuwa kipindi cha miaka 11, wamefanikiwa kuwafikia mamia ya wanaume kupitia programu mbalimbali, ikiwemo shughuli zilizofanyika katika shule za sekondari, vyuo vikuu pamoja na mikutano ya wanaume katika maeneo tofauti nchini.
Shing'oma ameeleza kuwa msingi wa uanaume bora hujengwa katika malezi, na pale malezi yanapokuwa na mapungufu, huathiri moja kwa moja aina ya mwanaume anayetarajiwa katika siku zijazo.
“Jamii yetu ina wanaume waliovunjika vipande vipande kutokana na namna walivyolelewa. Wengi hujifunza uanaume kwa kuangalia mfano wa baba, lakini wapo ambao hawakupata nafasi hiyo, hivyo hukosa mwongozo muhimu,” alifafanua.
Kwa mujibu wa shing'oma ameleza kuwa kumpata mwanaume bora ni mchakato unaohitaji malezi sahihi, mahusiano yenye kujenga na utayari wa kujifunza pamoja na kupokea maarifa mapya.
Aidha amefafanua kuwa kongamano hilo limeanzishwa baada ya tafiti mbalimbali kubaini changamoto zinazowakabili wanaume nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Matokeo ya tafiti hizo yalionyesha umuhimu wa kuwa na majukwaa ya wanaume kukutana, kujadiliana na kujengeana uwezo.
“Mwanaume ni kichwa cha familia. Ukimwacha nyuma mwanaume, umeiacha jamii yote nyuma. Ili taifa lipige hatua, ni lazima mwanaume awe katika nafasi yake kwa kupewa elimu, kukumbushwa wajibu wake na kupewa fursa sawa,” alisema.
Hata hivyo Shing'oma ameelwza faida za makongamano hayo ni pamoja na kuimarisha usalama wa familia, kukuza mitandao ya kibiashara na kuongeza kipato. Wanaume wanapokutana, hubadilishana mawazo ya biashara, uzoefu na mikakati ya kuboresha maisha yao kiuchumi.
Hata hivyo, changamoto za kihisia pia zimebainishwa kuwa mzigo mkubwa kwa wanaume wengi. Imeelezwa kuwa jamii imewajengea mtazamo kwamba mwanaume hapaswi kuonyesha hisia zao kwa kulia hali inayowafanya wengi kubeba maumivu kimya kimya.
“Wanaume wengi hulia ndani kwa ndani bila kuonekana hadharani. Hii imepelekea wengi kubeba majeraha ya muda mrefu,” aliongeza.
Aidha, imeelezwa kuwa pamoja na changamoto za unyanyasaji wa wanawake, kuna pia aina ya unyanyasaji wa kihisia unaofanywa dhidi ya wanaume, ambao nao umechangia kudhoofisha hali ya kisaikolojia na hadhi yao katika jamii.
Kwa ujumla, kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujenga uelewa mpya wa wanaume, kuimarisha mshikamano na kuweka mikakati ya pamoja ya maendeleo kwa wanaume na jamii kwa ujumla.
