Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI NYAISHOZI WAIOMBA SERIKALI KUWAPATIA MAJI SAFI

WANANCHI NYAISHOZI WAIOMBA SERIKALI KUWAPATIA MAJI SAFI

 

Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera

Wananchi wa vitongoji vya Kikungili, Omukajiji, Rushanje na Rwandalo kata ya Nyaishozi, wilayani Karagwe mkoani Kagera, wanalazimika kutumia maji yasiyo safi na salama kutoka kwenye dimbwi kwa matumizi ya nyumbani, kufuatia kuharibika kwa kisima walichokuwa wakikitumia takribani miaka mitatu.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakazi hao akiwemo Loveness Shubira amesema kuwa wanalazimika kutumia maji hayo ya dimbwi ambayo sio salama kutokana na kutokuwa na mbadala wake hivyo kuiomba serikali kuwasaidia kupata maji safi na salama .

“kwakweli tuna shida ya maji tunachota maji haya ya dimbwi ambayo sio safi kwahiyo tunaomba msaada ili tupate maji mazuri na masafi tunashida kubwa tunaomba watuangalie” 

Naye Alinjuna Domisian mkazi wa Kikungili amesema kuwa dimbwi hilo ni hatarishi kwa wakina mama na watoto ambao mara kadhaa wamekuwa wakidumbukia katika dimbwi hilo.

“tunayo changamoto ya maji katika maeneo haya tunatumia dimbwi hili ambalo wakati mwingine wakina mama na watoto huwa wanaanguka katika dimbwi hili kwahiyo tunaiomba serikali iweze kutungalia katika tatizo hili la maji”

Kwa upande wake Njunwa Fidel Mkazi wa Kitongoji Rushanje amesema kuwa awali walikuwa wanatumia kisima ambacho kwa sasa kimeharibika kwa muda mrefu zaidi ya miaka mitatu nyuma na kuiomba serikali kuwatengenezea kisima hicho.

“tulikuwa tunatumia kisima na baada ya kuharibika tukachimba dimbwi ambalo nalo maji yake sio salama lakini kwa sababu ya uhaba wa maji tunayatumia haya hali inayohatarisha afya zetu kwasababu watu wengi wanaugua matumbo kwa sababu ya haya maji”

Kadhalika wananchi hao wameiomba serikali kukamilisha haraka kwa mradi wa maji wa miji 28 wa Rwakajunju ambao wanatarajia utakuwa mkombozi kwao.

Akizungumza hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Karagwe Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa maji mhe.Kundo Mathew amesema kuwa mradi wa Rwakajuju ambao ulianza kutekelezwa tangu April mwaka 2023 na ulitarajiwa kukamilika mwezi Desember 2025 kwa sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake.

“serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi miwili ya maji katika mji wa Kayanga wilayani Karagwe ukiwemo mradi wa maji wa Rwakajunju unaotekelezwa kwa thamani ya shilingi bilioni 64.3 sambamba na mradi wa usambazaji wa maji wa katika mji wa Kayanga unaogharimu shilingi bilioni 1.3, mheshimiwa Naibu spika utekelezaji wa miradi hii umefikia asilimia 70”

Kukamilika kwa miradi hiyo inatarajiwa kuwanufaisha wananchi wapatao 356,790 wa wilaya ya Karagwe hali itakayo wasaidia wananchi wilayani kuondokana na adha ya kutumia maji ambayo sio safi na salama.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3