MWENYEKITI WA MTAA MBARONI KUUZA ENEO LA SHULE
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MKUU wa wilaya Kigoma Dk.Rashid Chuachua amemsimamisha uongozi Mwenyekiti wa Mtaa Mgeo kata ya Buhanda manispaa ya Kigoma Ujiji Azizi Ibrahim huku akitoa maelekezo kwa polisi kumkamata Mwenyekiti huyo na kumfungulia mashitaka ya tuhuma za kuingilia na kuuza eneo la shule ya Msingi Mgeo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma.
Dk.Chuachua alitoa maagizo hayo alipotembelea eneo lhilo la Shule kufuatia kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ya kuwepo kwa tuhuma za kuingiliwa kwa eneo la shule hiyo na kuuzwa kwa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Athanas Noel huku maelekezo ya Serikali kupitia Afisa Mtendaji wa kata ya Mgeo ya kusimamisha ujenzi huo yakipuuzwa.
Katika kauli yake kuhusu mgogoro huo Mkuu huyo wa wilaya Kigoma amemuagiza Mwanasheria wa Halmashauri ya manispaa ya Kigoma Ujiji kumtafuta na kumfungulia mashitaka Mwananchi aliyenunua eneo hilo, Athanas Noel kwa tuhuma za kuingia na kununua eneo la shule jambo ambalo ni kinyume cha sheria huku akiagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) kufungua jalada la uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika wote.
Awali akitoa taarifa kwa Mkuu wa wilaya Kigoma, Afisa Mtendaji wa kata ya Buhanda, Zeenat Ambikai alisema kuwa nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kuwa mtu huyo aliuziwa kiwanja hicho mwaka 2021 lakini alianza kujenga mwezi januari mwaka huu huku shule hiyo ikiwa imeanzishwa mwaka 2006.
Akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti huyo, Azizi Ibrahim alikiri kuuza kiwanja hicho akieleza kuwa awali akiwa mjumbe wa kamati ya ujenzi ya shule hiyo ramani ilikuwa inaonyesha kuwa sehemu ya kiwanja hicho ipo nje ya eneo la shule na ni mali ya wananchi.
Mwisho.



