WANANCHI KAGERA WASHAURIWA KUFANYA UCHUNGUZI WA AFYA ZAO MARA KWA MARA
Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Wananchi wa mkoa wa Kagera wamehimizwa kujenga utamaduni wa kufanya vipimo vya afya mara kwa mara, hatua itakayosaidia kugundua magonjwa mapema kabla hayajasababisha madhara makubwa, na hivyo kulinda nguvu kazi ya jamii.
Wito huo umetolewa na mkuu wa maabara kutoka hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera Bukoba Eustadius Kamugisha wakati wa ufunguzi wa wiki ya maabara nchini inayofanyika katika hospitali hiyo, inayoenda sambamba na huduma ya vipimo vya magonjwa mbalimbali bure kwa wananchi.
Aidha Kamugisha ameeleza kuwa miongoni mwa vipimo vinavyofanyika ni pamoja na vipimo vya ugonjwa wa figo, Ini, magonjwa ya shinikizo la damu,saratani ya mlango wa kizazi mkojo, vipimo vya damu na mengine huku akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kufanyiwa vipimo.
“tunafanya vipimo bure vya figo, shinikizo la damu vipimo vya ini, vipimo vya damu, tezi dume, saratani ya mlango wa kizazi, wingi wa damu, tunafanya vipimo hivi bure ili kuwawezesha hata wananchi wasiokuwa na uwezo wa kulipa hela kwa ajili ya kufanya vipimo vikubwa”
Kwa upande wake mratibu wa maabara mkoa wa Kagera, Emmanuel Mkumbo, amesema huduma zimeongezeka hadi zaidi ya vipimo 100 katika hospitali hiyo kutokana na uwekezaji wa serikali katika wataalamu na miundombinu.
“kwa sasa huduma za vipimo vikubwa katika hospitali ziongezeka mpaka kufika 100 kwa sasa tunauwezo wa kupima magonjwa tofauti tofauti na inawezesha wananchi kutotumia gharama kubwa kufuata huduma za vipimo vikubwa nje yam koa”
Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kufanya vipimo akiwemo Abdallah Muwazi na Neema Johanes wameshukuru kwa huduma hiyo ya kufanya vipimo bure kwa imewasaidia kujua afya zao na kwa imetakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi wasiokuwa na uwezo.
Wiki ya maabara nchini mkoa wa Kagera imeanza kuadhimishwa tangu April 20 na itafikia tamati April 24 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu isemayo “Utambuzi sahihi wa vipimo kwa matibabu bora ya magonjwa”




