WANANCHI BUKOBA WALILIA UJENZI WA KINGO ZA MTO KANONI
Apr 23, 2026
Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Wananchi wa kata nne kati ya saba zinazopitiwa na mto Kanoni manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wameiomba serikali kukamilisha ujenzi wa kingo za mto Kanoni, ili kuwaepusha na mafuriko ya mara kwa mara yanayowakumba wananchi hao hasa nyakati za masika.
Wakizungumza na vyombo vya habari akiwemo Khadija Omary mkazi wa Omukigusha kata ya Bilele emeeleza kuwa mafuriko yanayowakumba yamekuwa yakisababishwa na kufurika kwa mto Kanoni ambayo yanapelekea kupoteza mali na vyakula hivyo kuiomba serikali kuujengea mto huo ili kuwaepusha na mafuriko hayo.
“mafuriko yanapokuja yananiathiri sana tena sana kwangu mimi yakiingia kama sijajiandaa sitoi hata kimoja nguo na vyakula vinaloana juzi nimetoka kupoteza kilo 25 za unga baada yam aji kujaa ndani tunaiomba serikali ituangalie kwa jicho jingine”
Naye Speli Mwombeki amesema kuwa anaamini kuwa endapo kingo za mtu Kanoni zikikamilika wnanchi hao hawatakubwa ten ana mafuriko ya mara kwa mara katika makazi yao.
“shida kubwa huku ni mafuriko tumekuwa tunakumbwa na mafuriko ya mara kwa mara ila naamini kuwa kujengwa kwa kingo za mto Kanoni changamoto hii tutaondokana nayo”
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo mhandisi Emmanuel Festo ameeleza kuwa kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa kingo za mto Kanoni ni kutokana na mvua nyingi zinazonyesha katika mkoa wa Kagera na kuahidi kuwa ujenzi huo utaanza mwezi wa tano mwaka huu.
“mpaka sasaivi mkandarasi ameshindwa kufanya kazi kwa sababu ya mvua kubwa zinazonyesha katika mkoa huu ujenzi wa mto unahitaji kuchepusha maji, maji yanapokuwa mengi huwezi kuyachepusha ila tunatarajia mwezi wa tano mvua zitapungua na ujenzi utaanza”
Kata ambazo zimekuwa zikikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara katika manispaa ya Bukoba ni Bilele, Bakoba, Amgembe na Kagondo.
Ni miezi tisa sasa tangu kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kingo za mto Kanoni uliosainiwa mwezi wa saba mwaka 2025, ukitarajiwa kutekelezwa ndani ya mwaka mmoja chini ya kampuni ya kichina ya Shandong Luqiao Group lakini mpaka sasa ujenzi huo bado haujaanza.



