BUWASA,YAWACHUJA WAFANYAKAZI HODARI 2026, WATATU KUNG'ARA (MEI MOSI) KAGERA.
Apr 23, 2026
Na Matukio Daima News.
Kagera,Bukoba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), ameongoza kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Wafanyakazi kilicholenga kupitisha wafanyakazi hodari kwa mwaka 2026.
Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano Wa ofisi za mamlaka hiyo na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wa kamati hiyo waliokuwa na jukumu la kuchambua na kupendekeza majina ya watumishi bora kulingana na vigezo vilivyowekwa.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Wa Mamlaka hiyo Bw.John Sirati amewahimiza wajumbe kuhakikisha wanazingatia misingi ya utendaji kazi, nidhamu ya kazi, ubunifu katika majukumu, pamoja na kiwango cha uwajibikaji wa kila mtumishi na kusisitiza kuwa mchakato huo Wa chaguzi unapaswa kuwa wa haki na uwazi ili kuleta tija katika taasisi.
“Zingatieni kuwa wafanyakazi mtakaowachagua watakuwa chachu ya motisha kwa wengine, hivyo chagueni wale wanaoonesha mfano bora wa utumishi na wanaoweza kuhamasisha wenzao kufanya vizuri zaidi,” amesema Bw.Sirati.
Aidha, wajumbe wa kamati walipata fursa ya kujadili kwa kina utendaji wa wafanyakazi waliopendekezwa, wakizingatia mchango wao katika kufanikisha malengo ya Mamlaka hiyo, pia Majadiliano hayo yalilenga kuhakikisha kuwa wale watakaopitishwa wanawakilisha viwango bora vya utumishi wa umma.
Katika hatua nyingine, Baraza la Wafanyakazi BUWASA lilifanikiwa kupitisha jumla ya wafanyakazi watatu hodari ambao watapata nafasi ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka 2026 ngazi ya mkoa.
“Uteuzi huu ni matokeo ya kazi kubwa na juhudi za wafanyakazi wetu wanaojituma kila siku kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi, na tunatarajia wataendelea kuwa mfano kwa wengine,”
Maadhimisho ya (Mei Mosi )yanatarajiwa kufanyika katika Wilaya ya Missenyi, Mkoani Kagera na Kaulimbiu ya maadhimisho hayo Kwa mwaka huu ni “Kazi zenye staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” ikihimiza umuhimu wa kazi bora katika kufikia maendeleo ya muda mrefu ya taifa.

