WAKULIMA ACHANENI NA MBINU ZA ZAMANI KUONGEZA TIJA ZAO PAMBA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema wakulima wengi wa pamba nchini bado wanatumia mbinu za zamani za kilimo, hali inayochangia kushuka kwa uzalishaji licha ya baadhi yao kumiliki mashamba makubwa.
Chongolo ametoa kauli hiyo leo Aprili 16, 2026, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Pamba uliofanyika katika Jakaya Kikwete Convention Centre, akisisitiza umuhimu wa wakulima kuhamia kwenye matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na mapato.
Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wakulima pamoja na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema serikali imeboresha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo ili kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa gharama nafuu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
" Sera ya Kilimo ya mwaka 2023 inaelekeza kila kijiji kuwa na Afisa Ugani, ikiwa ni jitihada za kuwasaidia wakulima kupata ushauri wa kitaalamu na kufikia malengo ya kukuza uchumi wa mkulima ifikapo mwaka 2030," Amesema Waziri huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Marco Mtunga, amesema kuna haja ya kufanya maboresho ya kina katika mfumo wa ushirika ili kuongeza ufanisi katika tasnia hiyo.
Amefafanua kuwa bado kuna changamoto katika ugawaji wa pembejeo, matumizi sahihi ya mizani pamoja na usimamizi wa ubora wa pamba wakati wa mauzo, akieleza kuwa hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa mamlaka ya kutosha kwa wasimamizi wa vyama vya ushirika kuchukua hatua kwa wanaokiuka taratibu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emanuel Cherehani, ameishauri serikali kuunda mfumo madhubuti wa kusimamia vyama vya ushirika ili kuongeza tija kwa wakulima wa pamba nchini.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu isemayo “Nguvu ya Pamoja kwa Tasnia ya Pamba Endelevu,” ukilenga kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kukuza sekta ya pamba nchini.








