WADAU MBALIMBALI WASHIRIKI KATIKA KAMPENI YA CLEAN MOSHI CAMPAINGN ILIYOFANYIKA KATIKA MSITU WA RAU
Na Rehema Abraham, Moshi
Wadau kutoka taasisi mbalimbali wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kushiriki katika zoezi la kufanya usafi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuweka mazingira safi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Easy Amazing Tanzania, ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni ya Clean Moshi Campaign, amesema kuwa lengo lao ni kuonesha mchango wao kwa jamii katika kuifanya Moshi iwe bora zaidi na kuvutia.
Ameeleza kuwa uwepo wa mazingira safi katika mji wa Moshi ni fursa muhimu kwa vijana. Amesema vijana wengi wamekuwa wakihama na kwenda kutafuta fursa katika mikoa mingine, hivyo ni muhimu kutumia rasilimali zilizopo kujitengenezea ajira na fursa ndani ya mji huo.
Aidha, amesisitiza kuwa mojawapo ya njia ya kutumia fursa hizo ni kupinga uchafuzi wa mazingira kwa kauli mbiu kwamba “uchafu ni aibu,” hasa ikizingatiwa kuwa Moshi hupokea watalii wengi wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa wao kama wadau wa mazingira wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha kutambua umuhimu wa usafi, huku akisisitiza kuwa uchafu unapaswa kukataliwa na kila mmoja.
Pia amewataka wadau na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya kuonesha uwajibikaji na upendo kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za usafi, ili kuhakikisha mji wa Moshi unakuwa na mazingira safi na salama kwa wote.





