Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DKT.TULIA AZITEMBELEA FAMILIA ZILIZOATHIRIKA NA MAPOROMOKO RUNGWE, ATOA MSAADA

DKT.TULIA AZITEMBELEA FAMILIA ZILIZOATHIRIKA NA MAPOROMOKO RUNGWE, ATOA MSAADA

 


Na Matukio Daima Habari, Rungwe

SIMANZI na huzuni zimetanda kwa familia 11 zilizopoteza ndugu zao 22 kufuatia maafa ya maporomoko ya udongo yaliyotokea Machi 24, 2026 wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Spika Mstaafu wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), ametembelea familia hizo na kutoa msaada wa chakula pamoja na fedha ili kuwafariji wahanga.


Maporomoko hayo yaliyotokea majira ya saa saba usiku yalisababisha vifo vya watu 21 papo hapo, huku mtu mmoja akifariki baadaye kwa kunywa sumu kutokana na msongo wa mawazo baada ya kupoteza wajukuu zake watatu.


Akizungumza Aprili 1, 2026 wilayani humo, Dkt. Tulia amesema lengo la ziara hiyo ni kuwapa pole na faraja waathirika wa familia 11 zilizokumbwa na janga hilo, akibainisha kuwa mahitaji bado ni makubwa.

“Tumetembelea familia katika kata za Lupepo, Kinyara, Ikuti, Kawetele na Nkunga. Hali siyo nzuri—wengi wamepoteza makazi na wanaishi kwa majirani. Wanahitaji chakula, magodoro na makazi bora. Tunawaomba wadau kujitokeza kusaidia,” amesema.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa hatua za haraka zilizochukuliwa tangu kutokea kwa maafa hayo, huku akimpongeza uongozi wa wilaya kwa juhudi za awali za kuwahudumia waathirika.

Katika msaada huo, Dkt. Tulia alitoa kilo 440 za mchele na zaidi ya Sh milioni 4, ambapo kila familia ilipatiwa Sh 200,000 kulingana na ukubwa wa hasara, pamoja na kilo 20 za mchele kwa kila aliyepoteza ndugu.

“Niombe Watanzania tuendelee kujitokeza kusaidia. Tukishirikiana, tunaweza kupunguza uzito wa majonzi haya kwa wenzetu,” amesisitiza.

Mmoja wa waathirika, Joshua George, mkazi wa kata ya Kinyara aliyepoteza watoto wawili, alimshukuru Dkt. Tulia kwa msaada na faraja aliyotoa, akisema hatua hiyo imewapa nguvu katika kipindi kigumu wanachopitia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Rungwe, Mekson Mwakipunga, amesema tukio hilo limeacha majonzi makubwa, huku baadhi ya familia zikibaki bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maporomoko hayo.

Alieleza kuwa katika kijiji cha Mboyo, familia moja ilipoteza watu wanne, ambapo mmoja aliamua kunywa sumu baada ya kushindwa kuvumilia maumivu ya kupoteza wajukuu zake watatu.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3