VIJANA SAFINA STREET NETWORK MASHUJAA UCHANGIAJI DAMU MOROGORO
Na Matukio Daima, Morogoro
Katika juhudi za kukabiliana na uhaba wa damu nchini, watoto na vijana waliowahi kuishi mitaani na kwenye mazingira hatarishi wanaohudumiwa na mtandao wa Safina Street Network wameanza kuonekana kuwa msaada mkubwa kwa kushiriki kwa mwaka wa sita mfululizo katika uchangiaji wa damu kwa hiari.
Mtaalamu kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Daudi Mkawa amesema mahitaji ya damu bado ni makubwa huku mwitikio wa jamii ukiwa bado mdogo.
Mkawa alieleza kuwa Kanda ya Mashariki inayohusisha Mikoa ya Pwani, Dar es salaam na Morogoro kuna hospitali nyingi zikiwemo za rufaa zinaongoza kwa kuwa na mahitaji makubwa ya damu kutokana na idadi ya wagonjwa wanaohudumiwa ikiwemo kufanyiwa upasuaji, majeruhi wa ajali, kina mama wajawazito na watoto,wagonjwa wa Saratani na Upungufu wa damu (Sikoseli).
Amesema hatua ya vijana hao wa safina street network kuchangia damu kila mwaka imekuwa ni msaada mkubwa kwa benki ya damu, ambapo jumla ya vijana 100 walitarajiwa kushiriki zoezi hilo, na hadi mchana chupa sabini zilikuwa zimekusanywa katika zoezi lililokuwa bado linaendelea.
Akawaondoa hofu Wananchi kuwa Uchangiaji wa damu hauna madhara yeyote kiafya, na kwamba wamekuwa wakihakikisha usalama kwa wachangiaji ambao pia Wana faida mbalimbali ikiwemo kujua makundi ya damu na kupata cheti maalum kitakachowawezesha kupata mahitaji ya damu wakati wowote wakihitaji.
Mtaalamu huyo akasema damu ni Bure na haiuzwi badala yake ndugu wa mgonjwa mhitaji wa damu hupewa maelekezo ya kutafuta wachangiaji ili damu inayotolewa iendelee kusaidia akiba inayopunguzwa kwa faida ya wahitaji wengine.
Kwa upande wake, Mratibu wa Safina Street Network Morogoro, Amani Komba alisema wamekuwa wakiwajengea uwezo vijana hao na kuwashirikisha katika shughuli za kijamii.
Hata hivyo akasema Bado wanakabiliwa na changamoto ya Ubovu wa miundombinu ya barabara kufika kituo cha Morogoro na ukosefu wa umeme jambo linalowafanya kuishi katika mazingira magumu wakisubiri hisani ya Serikali pindi wakiwafikia.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Emmanuel Makoja akasema wamekuwa wakiwakusanya watoto wa mitaani kwa namna mbalimbali wakilenga kuwatoa mitaani, kuwaweka kwenye vituo na lengo kubwa ni kuwaunganisha na familia zao.
Aidha amesema wamewawezesha vijana hao kujiendeleza kimasomo na wengi wako elimu ya msingi, sekondari, Vyuo vya kati na Vyuo vikuu katika maeneo mbalimbali nchini, huku wengine tayari wamejitegemea kwa kujiajiri na kuajiriwa.
Akasema tangu vijana hao kuanza kujitolea kuchangia damu kwa kipindi cha miaka minne pekee tayari vijana zaidi ya mia nne wameweza kuchangia damu ambapo kwa mwaka huu pekee vijana 100 tayari wamechangia kwa hiari.
Makoja amesema suala la kuwasaidia watoto na vijana ni vyema likalenga kusaidia zaidi kwenye malezi, makuzi, ulinzi na usalama wa mtoto na kusisitiza ni wajibu wa kila mmoja hivyo ni vyema jamii zikiwemo taasisi za Serikali, binafsi na za dini wakaungana kuwasaidia.
Baadhi ya vijana, Selemani Nazareth ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa chuo huko mkoani Tanga amesema zoezi hilo linagusa maisha ya wananchi na ni zoezi salama ambalo halina changamoto zozote.
Naye Baraka Ismail mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesoma mafunzo ya ufundi huko Handeni mkoani Tanga amesema huu ni mwaka wa 12 tangu ameanza kuchangia damu na bado ana afya njema na akawashauri Watanzania wengine kutokuwa na hofu badala yake wajitokeze kufanya hivyo.
Mwisho




