IRAN YAIVIMBIA MAREKANI HAITAKI MAZUNGUMZO YA KUMALIZA VITA
Apr 4, 2026
Serikali ya Iran imetangaza rasmi kukataa masharti yote yaliyowekwa na Marekani kwa ajili ya kufanyika kwa mazungumzo ya kidiplomasia yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini Pakistan, hatua ambayo imeonekana kukwamisha juhudi za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kupunguza mvutano wa kijeshi unaoendelea.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tehran, viongozi wa Iran wamesema kuwa masharti yaliyowekwa na Marekani hayakubaliki na yanakiuka misingi ya mazungumzo ya usawa, hivyo hawatakuwa tayari kushiriki mazungumzo yoyote chini ya masharti hayo. Serikali ya Iran imesisitiza kuwa mazungumzo yanaweza kufanyika tuikiwa hakutakuwa na masharti ya awali kutoka upande wa Marekani.
Mazungumzo hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika nchini Pakistan, ambayo imekuwa ikijitokeza kama mpatanishi katika juhudi za kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili. Hata hivyo, uamuzi wa Iran kujiondoa katika mazungumzo hayo unatajwa kuwa pigo kubwa kwa juhudi za upatanishi zilizokuwa zinaendelea chini ya usimamizi wa Islamabad.
Vyanzo vya kidiplomasia vinaeleza kuwa Pakistan pamoja na wapatanishi wengine wa kikanda walikuwa wanajaribu kuandaa mkutano wa ana kwa ana kati ya maofisa wa Tehran na Washington kwa lengo la kujadili masuala ya usalama wa eneo, mivutano ya kijeshi, pamoja na suala la usafiri wa meli katika njia ya kimkakati ya Hormuz.
Lengo kubwa lilikuwa ni kufikia makubaliano ya awali ya kusitisha mashambulizi na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa vita ya wazi.
Hata hivyo, baada ya Iran kukataa masharti ya Marekani, kwa sasa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja yaliyopangwa kufanyika kati ya pande hizo mbili.
Wapatanishi wa kikanda sasa wanalazimika kutafuta mbinu mbadala za kufufua tena mchakato wa majadiliano, ikiwa ni pamoja na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kupitia nchi za tatu.
