Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
JUKWAA LA WAHARIRI LASIKITISHWA JAMBO TV KUFUNGIWA SIKU 90  LASHAURI HATUA MBADALA ZITUMIKE

JUKWAA LA WAHARIRI LASIKITISHWA JAMBO TV KUFUNGIWA SIKU 90 LASHAURI HATUA MBADALA ZITUMIKE

 


JUKWAA  la Wahariri Tanzania(TEF) limesikitishwa na uamuzi wa Serikali kukifungia kituo cha Jambo Online TV kwa muda wa siku 90.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema jukwaa linaamini iwapo kuna makosa ya kitaaluma (kama yapo) yaliyofanywa na mwanahabari mmoja, basi hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mhusika binafsi badala ya kuadhibu chombo kizima cha habari.


Tamko hilo la TEF linatolewa ikiwa imepita siku mbili tangu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilipotangaza kuifungia kwa siku 90 Jambo Online TV (kuanzia Aprili 2, 2026) kwa kile ilichoeleza kuwa imekuwa na mfululizo wa ukiukaji wa sheria, kanuni, masharti ya leseni, maadili, misingi na taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari.

Taarifa hiyo iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari, ilieleza sababu ya kufikia hatua hiyo ni kuwa kwa miezi minne mfululizo kuanzia Septemba 2025, Jambo Online TV kupitia akaunti zake za Instagram na chaneli yake ya utangazaji wa maudhui mtandaoni ya YouTube imekiuka taratibu hizo.

Dk Bakari alisema Machi 31, 2026, Jambo Online TV ilichapisha maudhui ambayo hakuwa na uhakika nayo na yasiyo na uthibitisho.


Maudhui hayo, amesema, yaliupotosha umma kuhusu hali ya matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na matokeo yanayotarajiwa kutoka Tume ya kuchunguza matukio wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kinyume na Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020 na marekebisho yake ya mwaka 2020 na 2025," amesema Dk Bakari

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3