FAMILY DAY KIDATU YAWAKUTANISHA POLISI NA WANANCHI KWA MICHEZO YA KIJAMII
Matukio Daima, Kilombero
WANANCHI wa maeneo ya Kidatu na viunga vyake wameungana na askari wa Jeshi la Polisi katika tamasha la Family Day lililofanyika katika Chuo cha Maafisa wa Polisi Tanzania (TPSC), tukio lililolenga kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Tamasha hilo limepambwa na michezo mbalimbali ya burudani ikiwemo kukimbia na magunia, kukimbiza kuku na kukimbia na mayai, iliyowavutia washiriki wa rika zote.
Kivutio kikuu kilikuwa ni fainali ya mpira wa miguu kati ya Polisi Kidatu na Polisi Ruhembe, ambapo timu hizo zilitoka sare ya 1–1 ndani ya dakika 90, kabla ya Ruhembe kushinda kwa penalti.
Akizungumza katika hafla ya kufunga tamasha hilo, Mkuu wa chuo cha maafisa wa Polisi Kidatu, SACP Zarau Mpangule, amesema kuwa matukio kama hayo yanaimarisha uhusiano kati ya polisi na jamii, jambo muhimu katika kudumisha amani.
Kwa upande wake,Mkuu wa Idara ya Michezo chuoni hapo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Amos Mikao amesema ushiriki mkubwa wa wananchi ni ishara ya mafanikio na kuahidi kuendeleza tamasha hilo siku zijazo.


