Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WATAALAMU WA USINGIZI NA GANZI WAIOMBA SERIKALI KUWALIPA SAA ZA ZIADA

WATAALAMU WA USINGIZI NA GANZI WAIOMBA SERIKALI KUWALIPA SAA ZA ZIADA

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma


WATAALAMU wa Huduma ya Usingizi na Ganzi nchini wameiomba serikali kuhakikisha wanalipwa kwa wakati malipo ya saa za ziada wanazofanya katika vituo vya afya, wakisema kucheleweshewa stahiki hizo kunapunguza ari ya kazi na kuhatarisha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Akizungumza katika kongamano la nne lililofanyika jijini Dodoma, rais wa Chama cha Wataalamu wa Dawa za Usingizi, Ganzi na Upasuaji Tanzania (TANPA), Dkt. Julia Mahamba, amesema kuwa uhaba wa wataalamu hao unawalazimu kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi ya kawaida, hasa katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto wakati wa upasuaji.


Amesema licha ya mchango wao mkubwa katika kuokoa maisha, bado wanakabiliwa na changamoto ya kutolipwa malipo ya saa za ziada kwa wakati.

“Tunafanya kazi kwa kujitolea kwa masaa mengi ili kuhakikisha huduma zinaendelea, lakini hatupati stahiki zetu kwa wakati hii inapunguza morali ya kazi na inaweza kuathiri ubora wa huduma,” alisema Dkt. Mahamba.

Pamoja na hayo, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zinazoendelea za kuimarisha sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na ajira mpya kwa wataalamu wa afya.


Kwa upande wake, Dkt. Evans Pesa ameeleza kuwa, kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu kwa wataalamu hao kujadili mikakati ya kuboresha huduma salama za usingizi na ganzi nchini kote, ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu.

Naye Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema serikali inatambua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa usingizi na ganzi, akibainisha kuwa kwa sasa kuna wataalamu takriban 2,950 wanaohudumia hospitali zaidi ya 800 nchini.

Ameongeza kuwa serikali imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na upungufu huo kwa kuongeza nafasi za mafunzo, hususan katika ngazi ya stashahada, ili kuongeza idadi ya wataalamu na kuboresha utoaji wa huduma.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wa kutosha watakaoweza kutoa huduma salama, kupunguza vifo vinavyotokana na upasuaji, hasa kwa mama na mtoto,” amesema.

Kwa ujumla, wataalamu hao wameisisitiza serikali kuzingatia ustawi wao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, wakiamini kuwa maboresho hayo yatachangia kuimarika kwa sekta ya afya nchini.





Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3