Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 CCM YATOLEA UVIVU UBADHIRIFU WA SARUJI HOSPITALI YA WILAYA KILINDI

CCM YATOLEA UVIVU UBADHIRIFU WA SARUJI HOSPITALI YA WILAYA KILINDI

.

NA AMINA SAIDI

MATUKIO DAIMA KILINDI.

​Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdrahman, ametoa onyo kali kuwa chama hicho hakitawafumbia macho watu wote wanaohusika na ubadhirifu wa fedha za serikali.

 Amesisitiza kuwa ni mwiko kutumia fedha za umma kwa manufaa binafsi badala ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.


​Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi.


 Katika ziara hiyo, ilibainika kuwepo kwa ubadhirifu wa mifuko ya saruji 145 iliyokuwa imehifadhiwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kuboresha huduma za afya wilayani humo.

​Mwenyekiti Rajabu alieleza kusikitishwa kwake na taarifa za wizi wa saruji pamoja na mingine kuharibika kwa  kuganda kutokana na kukaa muda mrefu bila kutumika.

 Alitaja hali hiyo kuwa ni uzembe wa wataalamu waliopewa dhamana ya kusimamia mradi huo na kushindwa kuwajibika ipasavyo.

​"Mradi huu wa Hospitali ya Wilaya Kilindi pesa yake imetolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 Kutokutumia vifaa hivi ipasavyo ni ubadhirifu wa pesa za serikali na kuwakosesha wananchi haki yao ya kupata huduma za afya, Kabla ya hapa wananchi walikuwa wanafuata huduma Morogoro, Handeni au Tanga mjini, jambo ambalo linawatia gharama kubwa," alisema Rajabu.


​Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti huyo ameagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ubadhirifu huo kwa njia moja au nyingine.


 Alisisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akielekeza mara kwa mara.


​Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, John Mgalula, amethibitisha kutokea kwa wizi huo na kueleza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa.


 Alisema walifanikiwa kumkamata dereva wa bodaboda akiwa na mifuko mitano ya saruji, jambo lililopelekea kukamatwa kwa mlinzi na fundi ambao kwa sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi zaidi.


​Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa baada ya kufanya ukaguzi, waligundua jumla ya mifuko 193 iliyokuwa na matatizo, ikijumuisha ile iliyoibiwa, iliyoganda, na iliyotumika kinyume na taratibu.


 Aliongeza kuwa bado wanafanya tathmini ya kina ndani ya stoo ili kubaini idadi kamili ya mifuko isiyofaa kabisa ili ujenzi uendelee.


​Licha ya changamoto hiyo, Mgalula amewahakikishia wananchi kuwa uongozi wa wilaya unafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha azma ya serikali ya kutoa huduma bora za afya kwa wakazi wa Kilindi inatimia bila vikwazo zaidi.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3