WAZIRI SANGU AHAMASISHA WANANCHI KUJIUNGA NA MFUKO WA TAIFA WA HIFADHI YA JAMII (NSSF)
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amewataka wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kujihakikishia usalama wa maisha yao ya baadaye.
Akizungumza katika uzinduzi wa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Waliojiajiri, uliofanyika katika Soko la Kimataifa la Dagaa la Mwaroni, lililopo wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza, Waziri Sangu alieleza kuwa sekta ya waliojiajiri inachukua nafasi kubwa katika uchumi wa Tanzania ambapo Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanafanya kazi katika sekta hii.
Waziri Sangu alisisitiza kuwa ili kufikia lengo la kuwa na mfumo wa hifadhi ya jamii unaowahudumia Watanzania wote, ni muhimu kuwafikia wananchi hao, hususani wale waliojiajiri na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imeanzisha mfuko wa skimu ya hifadhi kwa waliojiajiri, ambao unatoa fursa kwa wananchi, wavuvi, na wafanyabiashara.
"Serikali inaendelea kutafuta njia bora za kuwafikia wajasiriamali hawa ili waweze kunufaika na mafao ya hifadhi ya jamii," alisema Waziri Sangu.
Waziri Sangu alieleza kuwa mtu atakayekuwa amejiunga na NSSF na kuchangia mara kwa mara anakuwa na uhakika wa matibabu, msaada wakati wa matatizo, na kipato cha uzeeni. Aliongeza kuwa hifadhi ya jamii ni bima ya maisha ya baadaye.
"Tunapochangia, tunajiwekea bima kwa ajili ya maisha yako ya baadaye. Uchangiaji wa skimu hii unaanzia kwa kiwango cha chini cha shilingi 30,000 kwa mwezi, ambapo mtu anaweza kuchangia kidogo kidogo au kwa kiwango cha shilingi 5,200. Hiki ni kiwango rafiki, ambacho hata mjasiriamali mdogo anaweza kumudu na baadaye akafaidika na mafao ya mfuko wa jamii," alifafanua.
Waziri Sangu alisisitiza kuwa serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeanzisha skimu mahsusi kwa wavuvi na wafanyabiashara waliojiajiri.
Alisema kuwa ni muhimu kuwa na mfumo wa hifadhi wa jamii utakaowawezesha watu hawa kupata msaada wanapokutana na changamoto mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwahimiza wananchi kuona umuhimu wa kuhifadhi fedha kwa ajili ya kuweka akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye, hasa kwa ajili ya uzee.
Kwa upande wake, Masha Mshomba, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, alieleza kuwa serikali imeona umuhimu wa kuwahusisha wavuvi na wafanyabiashara katika mpango wa kuchangia katika mfuko wa hifadhi na kueleza faida zipatikanazo na kujiunga na mfuko huo ikiwa ni pamoja na kupata matibabu, msaada wa mazishi, na msaada wakati wa matatizo.
Erasto Barosha, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wauza Samaki wa Mwaroni, ambaye pia ni mmoja wa wanufaika wa mfuko huo, alieleza kuwa mfuko wa hifadhi umekuwa na manufaa makubwa kwao.
Aliiomba jamii kuendelea kujiunga na mfuko wa NSSF kwani utakuwa na manufaa makubwa kwao pindi wanapokutana na changamoto mbalimbali.
Kampeni hiyo yenye kauli mbiu isememayo Kampeni ya uzinduzi wa skimu hii inaongozwa na kauli mbiu isemayo: "Mipango Haistafu na Mazingira Hayana Likizo."






