HALMASHAURI YA IRINGA DC YAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE KWA MATENDO YA HURUMA KWA YATIMA ,YATOA MIKOPO TSH MILIONI 300
NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,IRINGA
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii, imeadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani kwa matendo ya huruma kwa kutoa misaada kwa vituo vya yatima vya Nzihi na Tosamaganga, pamoja na kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 300 kwa vikundi 26 vya wanawake na vijana.
Katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Saumu Kweka, alieleza kuwa mikopo hiyo inatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya Iringa DC na itatolewa bila riba kwa wanufaika.
Mikopo hiyo imekusudiwa kusaidia wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, na inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya kiuchumi ya jamii.
"Kwa niaba ya Halmashauri ya Iringa DC, tunajivunia kutoa mikopo hii kwa vikundi mbalimbali vya wanawake na vijana Mikopo hii ni ya kipekee kwani haina riba, na inatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri tunajivunia kuona wanawake na vijana wanapata fursa ya kuboresha maisha yao kupitia mikopo hii," alisema Kweka.
Aliongeza kuwa hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali kuendelea kuwawezesha wanawake na makundi mengine kupitia mikopo hii ya asimilia 10, inayolenga kuwasaidia watu walio katika hali ya uhitaji.
Kweka alikishukuru serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya wanawake na makundi mengine kupitia fursa mbalimbali za kifedha.
Aidha Kweka alisema idara hiyo inaendelea kutekeleza malengo na mipango yote na maelekezo yanayotolewa na waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima.
Mbali na mikopo, Halmashauri ya Iringa DC pia iliwatembelea watoto yatima katika vituo vya Nzihi na Tosamaganga, na kutoa misaada ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.
Hatua hii ililenga kuonyesha upendo na msaada kwa watoto yatima, sambamba na kuadhimisha Siku ya Mwanamke.
"Matendo ya huruma kwa watoto hawa yatima ni sehemu ya juhudi zetu za kuonyesha upendo na mshikamano kwa makundi yaliyosahaulika katika jamii. Tunataka kuwaonyesha kwamba sote tuko pamoja katika kujenga jamii yenye haki na usawa," alieleza Kweka.
Maadhimisho haya ya Siku ya Mwanamke kwa Halmashauri ya Iringa DC yamehitimishwa kwa kongamano la kitaifa kuhusu haki za wanawake, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta.
Katika kongamano hilo, Sitta aliwasihi wananchi wa Iringa kuendelea kupigana dhidi ya ukatili wa kijinsia, na kuhimiza jamii kutoa elimu kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia ili kuondoa mila potofu zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
"Mikakati ya kupambana na ukatili wa kijinsia ni muhimu ili kuhakikisha wanawake wanakuwa salama na wanapata haki zao tunapaswa kuendelea kutoa elimu na kufanyakazi kwa pamoja kuondoa ukatili huu katika jamii yetu," alisema Sitta.
Aliongeza kuwa, serikali inaendelea kutoa mikakati na sera madhubuti za kuendeleza haki za wanawake, vijana na watoto, na kuhakikisha kuwa jamii inajengeka kuwa na usawa wa kijinsia.
Kongamano hili lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kijamii, na wanajamii wa Iringa.
Siku ya Mwanamke Duniani ilikumbusha umma kuhusu mchango mkubwa wa wanawake katika jamii na umuhimu wa kuhakikisha wanapata haki sawa katika nyanja zote za maisha.
Halmashauri ya Iringa DC inatarajia kuendelea na jitihada hizi za kuwawezesha wanawake, vijana, na makundi mengine kwa kupitia mikopo, elimu, na msaada wa kijamii.
.jpg)







.jpg)




