BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA YATEKELEZA MIRADI YA MAJI KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MAJI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
BODI ya Maji Bonde la Ziwa Victoria imesema inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za maji katika maeneo ya bonde la Ziwa Victoria ili kuhakikisha matumizi endelevu ya maji kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya kiuchumi.
Hayo yameelezwa Machi 6, 2026 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa bodi hiyo, Renatus James Shinhu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo Mtumba kuhusu utekelezaji wa miradi ya mwaka wa fedha 2025/26.
Dkt. Shinhu amesema bodi hiyo ina jukumu la kusimamia, kulinda na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za maji katika bonde hilo kupitia ukaguzi na ufuatiliaji wa matumizi ya maji katika mito, mabwawa pamoja na vyanzo vingine vya maji.
“Tunaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kwa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa matumizi ya maji katika mito, mabwawa na vyanzo vingine ili kuhakikisha matumizi yake yanafanyika kwa uendelevu,” amesema Dkt. Shinhu.
Amesema kupitia mradi wa utafiti na uchimbaji wa visima, bodi imefanya tafiti za maji chini ya ardhi katika mikoa ya Simiyu Region, Mwanza Region, Mara Region na Kagera Region pamoja na kusimamia uchimbaji wa visima na ujenzi wa miundombinu ya maji katika maeneo husika.
Aidha amesema kupitia mradi wa ujenzi wa mabwawa, bodi imejenga mabwawa mawili katika wilaya ya Maswa District likiwemo bwawa la Bugarama lililopo kata ya Iyogelo na bwawa la Mwamashindike lililopo kata ya Mwabaraturu.
Amefafanua kuwa mabwawa hayo yanatumika kwa matumizi ya binadamu, mifugo na kilimo cha umwagiliaji, hali inayosaidia kuongeza upatikanaji wa maji na kuimarisha shughuli za uzalishaji katika maeneo hayo.
Kwa upande wa ufuatiliaji wa rasilimali za maji, bodi imesimika vituo maalum vya kufuatilia mwenendo wa maji katika mito ya Duma, Mori, Ngono, Mwisa na Kagera (Nyakanyasi), pamoja na mabwawa ya New Sola na Manchira na kituo kimoja katika Lake Victoria.
“Vituo hivi vinakusanya takwimu za mtiririko, ujazo na kina cha maji ambazo hutusaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu mafuriko, ukame na upangaji wa matumizi ya maji,” ameongeza Dkt. Shinhu.
Pia bodi imetunza jumla ya vyanzo vya maji 25 kwa kuviwekea mipaka ya kudumu na mabango ya tahadhari huku vyanzo sita vikiombewa kutangazwa rasmi kuwa maeneo tengefu, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kulinda vyanzo vya maji na kuepuka uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya bonde la Ziwa Victoria.
.jpg)