Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WANANCHI IRINGA WAASWA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI

WANANCHI IRINGA WAASWA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI

 

Mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Linda Selekwa ambae ni mkuu wa wilaya ya Mufindi akifungua mkutano wa wadau wa mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) kutoa kulia ni mstahiki meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada ,mkurugenzi wa IRUWASA mhandisi David Palangyo na kushoto ni Mkurugenzi wa bodi ya IRUWASA Monica Mbega picha na Matukio Daima Media

Na Matukio Daima Media,Iringa .

Wananchi mkoani Iringa wameaswa kutumia maji kwa uangalifu na kutunza vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, wakati wa mkutano wa wadau wa IRUWASA uliofanyika mkoani hapa.

Dkt. Salekwa alisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na miundombinu yake, akipongeza mikakati ya miaka mitano ya mamlaka hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Alisema elimu kwa umma ni muhimu ili kuwafanya wananchi watambue athari za vitendo vinavyoharibu mazingira na vyanzo vya maji, sasa na kwa vizazi vijavyo.

“Kuna umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na athari za uharibifu wa mazingira. Elimu itasaidia kubadili mtazamo na tabia,” alisema.


Aidha, alieleza kuwa mkoa unaendelea kuhamasisha upandaji miti, hususan katika maeneo ya vyanzo vya maji, akibainisha kuwa kila mwaka mkoa umefanikiwa kuvuka malengo ya upandaji miti kutokana na ushirikiano kati ya serikali na wananchi.

Aliongeza kuwa IRUWASA imekuwa ikiwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuboresha huduma ya maji na kupunguza umbali wa kufuata huduma hiyo, hatua inayounga mkono juhudi za Rais za kumtua mama ndoo kichwani.

Pia alibainisha kuwa mamlaka hiyo imeanzisha vyanzo mbadala vya maji vyenye uhakika ili kuhakikisha miradi inakuwa endelevu na haikumbwi na changamoto ya kukauka kwa vyanzo wakati wa kiangazi.

Mpango mkakati wa miaka mitano wa IRUWASA wa kuanzia Julai 2026 hadi Juni 2031 unalenga kuimarisha upatikanaji wa maji wakati wa majanga kama mafuriko na ukame, pamoja na kuboresha miundombinu kwa kuweka mabomba imara katika maeneo yenye mabomba chakavu au yaliyopasuka.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kwakilosa, Hamid Mbatta, aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji na kutimiza wajibu wao kwa kulipa bili kwa wakati ili kuwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora.

Alisema uharibifu wa vyanzo vya maji unaweza kuathiri hadhi ya mamlaka hiyo, ambayo imekuwa miongoni mwa mamlaka bora nchini kwa miaka mitano mfululizo.

Awali, akiwasilisha mpango wa biashara wa miaka mitano, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa IRUWASA, Jessica Mwalyoyo, alisema mamlaka hiyo ni miongoni mwa mamlaka sita zilizo katika daraja la ‘AA’, zenye jukumu la kutoa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa na maeneo ya pembezoni.

Alifafanua kuwa mamlaka zilizo katika daraja la ‘AA’ zinatakiwa kujiendesha bila kutegemea ruzuku ya serikali, kwa kugharamia uendeshaji, matengenezo, ukarabati wa miundombinu, maslahi ya watumishi pamoja na uwekezaji.

“Kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, tunapaswa kuimarisha ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya rasilimali,” alisema.

Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3