UMUHIMU WA RAMADHANI KWA ISLAMU
Na Ester Sebastian, Matukio Daima Media
Waumini wa dini ya Kiislamu katika Msikiti wa Masjid Luqman, uliopo katika mkoa wa Iringa, wameeleza umuhimu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kama kipindi cha toba na kujitahidi kuacha mambo yote yanayochukiza Mwenyezi Mungu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kasim Bakari, mmoja wa waumini wa Msikiti huo, amesema kuwa Ramadhani ni mwezi wa kipekee kwa Waislamu, ambapo kila muumini anapaswa kufunga ili kutubu na kurudi kwa Allah kwa kumtukuza na kumuomba msamaha kwa makosa waliyo ya fanya.
"Mwezi huu ni mtukufu, na kila jambo zuri linalofanywa katika mwezi huu lina thawabu nyingi zaidi. Waislamu wanatakiwa kujitahidi kufanya ibada, kusoma Qur'an, na kuacha mambo yote yaliyo haramu ambayo Allah ameyakataza. Pia, kila tendo la kheri linazawadiwa mara kumi katika mwezi huu," alisema Bakari.
Vilevile, Warda Mossi, mkazi wa Tumaini na muumini wa Msikiti wa Luqman, alieleza kuwa Ramadhani ni mwezi wa muhimu kwa wanawake na wasichana, kwani ni fursa ya kuomba toba na kufanya matendo mema ili kupata neema kutoka kwa Allah. Alisema kuwa wanawake wanaoshiriki katika kufunga wanapata faida kubwa kiroho, lakini pia alizungumzia changamoto zinazowakumba baadhi ya wanawake katika kipindi hiki.
"Kuna wanawake ambao hawatakiwi kufunga kwa sababu ya hali zao za kimaisha kama vile wajawazito, wanaonyonyesha, na wale walioko katika kipindi cha hedhi. Lakini, kwa wanawake wengine ambao hawana changamoto yoyote ya kimwili, wanatakiwa kufunga ili waweze kutubu na kuomba msamaha kwa Allah," alieleza Mossi.
Ramadhani ni kipindi cha kipekee ambapo Waislamu hutafuta neema za Allah kwa kufanya matendo ya kheri, kufunga, na kujiepusha na dhambi. Ni wakati wa kujenga imani na kujiweka karibu na Mungu, huku pia wakijizatiti kufanya ibada na kutafuta msamaha wa dhambi zao.
MWISHO
