MOI YATIMIZA MIAKA 30, YAOKOA FEDHA ZA RUFANI NJE YA NCHI KWA HUDUMA ZA KIBOBEZI
Na Hamida Ramadhan Matukio Daima Media Dodoma
WAKATI Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) ikitimiza miaka 30 ya utoaji wa huduma za kibingwa, uongozi wake umetangaza mafanikio makubwa yaliyopatikana mwaka 2025, yakionesha mwelekeo mpya wa kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya nchi na kuimarisha ubora wa tiba nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, alisema taasisi hiyo imeendelea kuwa kitovu cha huduma za ubongo, uti wa mgongo, mishipa ya fahamu na mifupa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Katika kipindi cha mwaka mmoja, tumeweza kupiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibobezi ambazo hapo awali zilihitaji wagonjwa kwenda nje ya nchi leo hii, huduma hizo zinapatikana hapa hapa Tanzania,” alisema Dkt. Ulisubisya.
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2025, MOI imehudumia wagonjwa 176,987 wa nje na dharura (OPD na EMD), huku wagonjwa 9,922 wakipatiwa matibabu ya kulazwa (IPD), takwimu zinazoonesha kuongezeka kwa mahitaji ya huduma hizo nchini.
Miongoni mwa mafanikio makubwa ya mwaka huo ni kuanzishwa kwa huduma mpya tisa za kibobezi, zikiwemo upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde, upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu na tiba ya maumivu sugu.
“Kuanzishwa kwa huduma hizi kumeokoa fedha nyingi za kigeni na kupunguza mateso kwa wagonjwa na familia zao waliokuwa wakilazimika kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu,” alisisitiza.
Aidha, MOI imeimarisha huduma za upandikizaji wa nyonga na magoti bandia, upasuaji wa mishipa ya damu kwenye ubongo bila kufungua fuvu na matibabu ya kiharusi kupitia mishipa mikubwa ya damu.
Katika mwaka huo, wagonjwa 2,228 walipatiwa huduma za kibobezi za hali ya juu, huku wagonjwa 31 wakifanyiwa upasuaji wa marudio wa nyonga na magoti, mafanikio yanayoonesha kuongezeka kwa utaalamu wa ndani.
Amesema MOI imeanza rasmi wodi maalum za kisasa (Premier Ward) zenye vyumba 25 kwa ajili ya wagonjwa maalum na wa kimataifa, ikilenga kuboresha hadhi ya huduma na kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, wagonjwa wa kimataifa waliopatiwa huduma mwaka 2025 walitoka katika nchi za Congo, Comoro, Uganda, South Sudan na Burundi.
“Hii inaonesha wazi kuwa MOI sasa ni kituo cha rufaa cha kikanda, na tunajivunia kuiletea Tanzania heshima katika sekta ya afya,” amesema.
Mbali na huduma za tiba, MOI inaendelea na miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la OPD lenye thamani ya shilingi bilioni 13.8, ambalo likikamilika litaongeza uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 1,500 kwa siku.
Katika kuimarisha rasilimali watu, taasisi imeajiri watumishi 26 na kusomesha madaktari bingwa tisa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
MOI pia ni hospitali ya kufundishia ya College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA) na College of Anaesthesiologists of East, Central and Southern Africa (CANECSA).
“Tunaendelea kuboresha huduma zetu kwa viwango vya kimataifa na tuna mipango ya kujenga hospitali ya kisasa ya utengamao Mbweni ili kuhakikisha Watanzania wanapata matibabu bora bila kulazimika kwenda nje ya nchi,” amehitimisha Dkt. UlisubisyaAmesema</
p>









