UGONJWA PID WATESA WANAWAKE WENGI
Na Angelina Mbunda (UoI) – MATUKIO DAIMA
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Ilembula, inayopatikana katika Chuo Kikuu cha Tumaini, mkoani Iringa, ameeleza sababu zinazochangia kuenea kwa ugonjwa wa PID (Pelvic Inflammatory Disease) kwa wanawake, hususan kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24.
Akiwa ofisini kwake, mganga huyo amesema kuwa sababu hizo huchangia changamoto kubwa katika afya ya uzazi ya wanawake, huku akielezea kwa undani athari zinazoweza kutokana na ugonjwa huu.
Amesema kuwa, kabla ya kueleza sababu za PID, ni muhimu kuelewa kwamba ugonjwa huu una aina mbili:
PID ya muda mfupi (ambayo haijakomaa), ambayo hutibika kwa haraka kwa kutumia dawa za Antibiotics.
PID ya muda mrefu (PID iliyo komaa), ambayo huchukua muda mrefu kutibika na inaweza kuwa na madhara makubwa kwa mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Mganga huyo alibainisha kuwa, bakteria wawili ambao husababisha PID ni N. gonorrhea na Chlamydia, bakteria hawa wanaweza kuathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke.
Sababu nyingine ni kuwa na historia ya magonjwa ya zinaa (STIs), matumizi ya vidonge vya mpango wa uzazi, kuwa na wapenzi wengi, na matumizi ya sabuni zenye kemikali kuosha sehemu za siri.
Alisema, “Mwaka 2013, wanawake elfu themanini waligundulika kuwa na maambukizi ya PID hata hapa nyumbani kwetu, wapo wanawake wanaoishi na PID lakini hawafuatilii matibabu kwa haraka, jambo linaloweza kuleta madhara makubwa,” alisema.
Waziri wa Afya na Mazingira Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu cha Iringa, Michael Nchimbi, ambaye pia ni mwanafunzi wa Sheria mwaka wa tatu, aliongeza kuwa, “Sababu nyingine zinazochangia PID ni kufanya baadhi ya taratibu za kiafya bila usafi wa kutosha, kama vile upimaji wa ndani wa kizazi, kutotumia kinga wakati wa tendo la ndoa, na utoaji wa mimba kiholela kwa kutumia madawa yenye kemikali.”
Alisisitiza kuwa uelewa mdogo wa afya ya uzazi na imani potofu kama "kufanya mapenzi mara ya kwanza au mara moja huwezi kupata maambukizi ya STIs" ni miongoni mwa sababu zinazoongeza hatari ya PID kwa vijana.
Fatuma Ndau, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa anayejiandaa kwa shahada ya pili ya Psychology, alieleza kwamba majeraha katika uke au mlango wa uzazi yanaweza kutokea wakati wa ngono ya nguvu, ubakaji, au matumizi ya vifaa visivyofaa.
“Kujifungua katika mazingira yasiyo salama, hasa kwa wasichana wadogo wanaojifungua bila msaada wa wahudumu wa afya, pia huongeza hatari ya PID,” aliongeza Fatuma.
Veronica Sanga, mwanafunzi wa Shahada ya Pili ya Maendeleo ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Iringa, alisema kuwa mabadiliko ya homoni yanayotokea katika umri wa kubalehe pia yanaweza kuathiri mfumo wa uzazi wa mwanamke.
“Usafi duni wa sehemu za siri, kutonawa vizuri au kutumia vifaa visivyo safi wakati wa kijisitiri huongeza hatari ya PID,” alieleza Veronica.
Pia aliongezea kuwa, unyanyapaa na hofu ya kutafuta huduma za afya ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokumba wanawake.
Wengi huogopa kuhukumiwa na jamii au wahudumu wa afya, na kwa hiyo kuchelewa kutafuta huduma za afya hali hii inachangia kuongezeka kwa athari za PID.
“Wanafunzi wengi wakiwa katika hali ya umasikini na utegemezi wa fedha kwa wenza wa ngono, pia wanakutana na vikwazo vya kutafuta huduma bora za afya,” alisema Veronica.
Katika kumalizia, wataalamu hawa walisisitiza kuwa elimu ya afya ya uzazi, vipimo vya mara kwa mara, na matumizi ya kinga kama kondomu ni silaha muhimu katika kupambana na PID.
Elimu hii inahitajika ili kupunguza maambukizi ya PID, ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa kama vile maumivu ya maisha, kupoteza uwezo wa kupata watoto, na madhara mengine ya kiafya.
Matokeo Chanya ya Elimu ya Afya ya Uzazi: Ni muhimu kwa wanawake, hasa vijana, kufahamu athari za PID na kutafuta matibabu kwa haraka.
Kupitia elimu na ufahamu sahihi, tunaweza kupambana na tatizo hili linaloathiri wanawake wengi, hasa vijana wenye umri wa miaka 15-24.

