Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
TAKUKURU YAOMBWA KUCHUNGUZA UFUJAJI WA FEDHA KATIKA TAASISI ZA DINI ‎

TAKUKURU YAOMBWA KUCHUNGUZA UFUJAJI WA FEDHA KATIKA TAASISI ZA DINI ‎

 

‎Na Elisante John, Singida.

‎Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeombwa kuzifanyia uchunguzi taasisi za dini nchini ili kubaini vitendo vya ufujaji wa fedha za sadaka, miradi ya maendeleo, na michango mingine, vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi kinyume na taratibu za madhehebu husika.

‎Ombi hilo limetolewa na Alhaji Shekhe wa Mkoa wa Singida, Issah Nassoro, katika hafla ya futari iliyoandaliwa na TAKUKURU kwa waumini wa Kiislamu pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani humo.

‎Alhaji shekhe Issah Nassoro amesema kwa sasa kumekuwapo dalili za ongezeko la ufujaji wa fedha ndani ya taasisi za dini, hali inayodaiwa kuhitaji taasisi hiyo kuingilia kati kwa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.


‎Amesema hatua hiyo itasaidia kufyeka vitendo visivyofaa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa dini wasiokuwa waaminifu katika usimamizi wa rasilimali za waumini.

‎“Msione ajabu siku hizi hata baadhi ya viongozi wa dini wanahusishwa na vitendo vya rushwa. Badala ya sisi kuwa mstari wa mbele kuwakemea viongozi wa serikali, imefikia hatua sisi wenyewe tunaonywa kuhusu tatizo hili,” alisema alhaji Shekhe Nassoro.

‎Aliongeza kuwa ndani ya nyumba za ibada kuna mambo yasiyo halali yanayodaiwa kufanyika, ikiwamo ubadhirifu wa fedha za waumini kupitia michango ya sadaka, na kuwataka TAKUKURU kutosita kufanya uchunguzi katika maeneo hayo.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliipongeza TAKUKURU kwa ubunifu wa kutoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa kupitia utaratibu wa futari kwa makundi mbalimbali ya jamii.


‎Amesema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za rushwa, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi hiyo kuendelea kuimarisha mbinu na weledi katika kukabiliana na changamoto hiyo.

‎Aidha, aliwataka wananchi kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kulinda ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa taifa.

‎Naye Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Petro Horombe, alisema ushirikiano wa wananchi unabaki kuwa nguzo muhimu katika kufichua na kuzuia vitendo vya rushwa vinavyoweza kudhoofisha maendeleo.

‎Kwa upande wao, baadhi ya wadau waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Mkoa wa Singida, Askofu Amosi Maghasi wa Kanisa la FPCT Kibaoni, walisema elimu inayotolewa na TAKUKURU imeongeza uelewa wa wananchi kuhusu madhara ya rushwa.

‎Askofu Maghasi ameahidi kuwa kamati yake itaendelea kushirikiana na TAKUKURU katika kuimarisha umoja na mshikamano, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vinavyochochea rushwa.

‎Askofu Maghasi ameahidi kuwa kamati yake itaendelea kushirikiana na TAKUKURU katika kuimarisha umoja na mshikamano, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya vitendo vinavyochochea rushwa nchini.

‎Hafla hiyo ya futari imelenga kuimarisha uhusiano kati ya TAKUKURU na wadau wake, pamoja na kujadili mikakati madhubuti ya kuendeleza vita dhidi ya rushwa ili kujenga jamii yenye uadilifu, uwajibikaji na maendeleo endelevu nchini.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3