SHEIKH DODOMA AHIMIZA WAISLAMU KUENDELEZA MAADILI BAADA YA RAMADHANI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SHEIKH wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mustapha Rajabu, amewahimiza waumini wa Kiislamu kuendeleza maadili mema waliyojifunza wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, akisisitiza kuwa swaumu haina maana iwapo mtu atarejea katika matendo maovu mara baada ya kumalizika kwake.
Akihutubia waumini katika swala ya Idd El Fitri iliyofanyika Msikiti wa Gaddafi jijini Dodoma, Jumamosi Machi 21, Sheikh Rajabu amesema Ramadhani ni kama chuo maalum cha mafunzo ya kiimani na nidhamu ya maisha, hivyo mafundisho yake yanapaswa kuendelea kuonekana katika maisha ya kila siku.
Ameonya kuwa kurejea kwenye chokochoko, migogoro na vitendo visivyo na maadili ni sawa na kupoteza dhamira ya swaumu.
“Tutakaporuhusu chokochoko, tutakuwa tumebaki na njaa tu bila faida ya kiroho Ramadhani ilikuwa ni kipindi cha kupanda mbegu za imani, uvumilivu na amani ndani ya nafsi zetu,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa swaumu humjengea mtu kinga dhidi ya maovu, lakini kinga hiyo inahitaji kulindwa kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kujiepusha na matusi, ugomvi na mienendo inayoweza kuvuruga amani ya jamii.
Amesisitiza kuwa Muislamu wa kweli hupimwa kwa matendo yake, akibainisha kuwa ni yule ambaye watu wengine wanakuwa salama kutokana na ulimi na mwenendo wake.
Katika hatua nyingine, Sheikh Rajabu amewakumbusha waumini kuwa ibada na maadili ya Ramadhani hayapaswi kuishia ndani ya mwezi huo pekee, bali yaendelee katika mwaka mzima, ikiwa ni pamoja na kuendeleza usomaji wa Qur’an, mshikamano na upendo katika jamii.
Pia ametoa wito kwa waumini kujiepusha na mifano mibaya ya migogoro inayoendelea katika baadhi ya maeneo duniani, na badala yake waendelee kuilinda na kuienzi amani waliyoijenga wakati wa Ramadhani.
“Tusiruhusu amani yetu ivunjike tuendelee kuishi kwa upendo na kuheshimiana kila siku, si wakati wa Ramadhani pekee,” amesisitiza.
Mwisho
