SERIKALI KUANZISHA PORTAL YA KIDIJITALI KURAHISISHA MATUMIZI YA TAFITI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WANANCHI na wadau wa maendeleo nchini wanatarajia kunufaika na matumizi bora ya tafiti kufuatia mpango wa Serikali wa kuanzisha mfumo wa kidijitali (portal) utakaorahisisha upatikanaji na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanyika nchini.
Kupitia mfumo huo, tafiti ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikibaki kwenye makabrasha au taasisi husika, sasa zinatarajiwa kuwa wazi, rahisi kupatikana na kutumika moja kwa moja katika kufanya maamuzi ya kisera na kupanga mipango ya maendeleo.
Akizungumza jijini Dodoma Machi 23, 2026 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kitaifa wa taasisi za utafiti, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt,Tausi Kida, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi ya kimkakati ya kuifanya Tanzania itumie maarifa na ushahidi katika kujenga uchumi imara.
Ameeleza kuwa mfumo huo utaimarisha uwazi, kuongeza ushirikishwaji wa wadau, na kuhakikisha tafiti zinatumika kutatua changamoto halisi za wananchi.
“Tunahitaji tafiti zinazojibu mahitaji ya Watanzania na kusaidia kuunda sera zenye tija. Mfumo huu utakuwa kiunganishi muhimu kati ya watafiti na watunga sera,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt, Kida amebainisha kuwa Tanzania ipo kwenye mkondo muhimu wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa trilioni moja na kuinua ustawi wa wananchi.
Amesema dira hiyo inalenga pia kutokomeza umasikini uliokithiri, kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga, pamoja na kuboresha huduma za msingi kama afya na elimu.
“Tutahakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa dira hiyo utafanyika kupitia mipango ya muda mrefu itakayogawanywa katika vipindi vya miaka mitano mitano, huku kila mwaka ukiwa na vipaumbele maalum vya utekelezaji.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji Mipango ya Kitaifa, Dkt, Mursali Milanzi, amesema Tume ya Taifa ya Mipango ina jukumu muhimu la kusimamia mwelekeo wa uchumi wa nchi kwa kuchambua masuala kama mfumuko wa bei, mapato na matumizi ya Serikali, pamoja na kuhakikisha ukuaji endelevu.
Ameongeza kuwa Tume pia inaratibu mipango ya maendeleo katika ngazi zote ili kuhakikisha inalingana na malengo ya taifa na kuepusha migongano ya utekelezaji.
Mkutano huo wa siku mbili unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za utafiti, ili tafiti zinazofanyika ziendane moja kwa moja na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.
Kwa ujumla, hatua hiyo inaashiria mwelekeo mpya wa Tanzania katika kutumia tafiti kama nyenzo kuu ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii, huku ikilenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaowanufaisha wananchi wote.
.jpg)

