Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
RC MALIMA   AONYA WANAOTUMIA VYANDARUA KUFUGIA KUKU NA KUVULIA SAMAKI MOROGORO

RC MALIMA AONYA WANAOTUMIA VYANDARUA KUFUGIA KUKU NA KUVULIA SAMAKI MOROGORO

📌 Bilioni 19 zatengwa kupambana na Malaria nchini

Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaMedia


Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya Malaria nchini, ambapo kati ya fedha hizo, bilioni 15 zitatumika kwa ununuzi wa viuatilifu katika kiwanda cha Kibaha na kusambazwa katika halmashauri 184.

Fedha hizo zimetengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026.

Hayo yamebainishwa mkoani Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika halmashauri saba zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria.

Mratibu wa Malaria na Mdhibiti wa Wadudu Waharibifu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Stella Kajenge, amesema kuwa kati ya bilioni 19 zilizotolewa, bilioni 4 zimetumika kununua pampu za kunyunyizia viuatilifu ambazo zitasambazwa katika halmashauri zote nchini.

Aidha, Kajenge alieleza kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI imetoa mwongozo wa kitaifa wa mapambano dhidi ya malaria unaohusisha sekta mbalimbali, kutokana na ukweli kuwa shughuli kama kilimo, ufugaji na ujenzi zinaweza kuchangia kuzalisha mazalia ya mbu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Logistics kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Hassan Ibrahim, alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020 walifanikiwa kusambaza vyandarua katika mikoa 10, vikifikishwa katika halmashauri 50 na kufikia zaidi ya vyandarua milioni 16.

Aliongeza kuwa zoezi hilo lilifanyika kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, huku kwa Mkoa wa Morogoro pekee wakitumia magari 30 kurahisisha usambazaji.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alisema kuwa Serikali itasambaza jumla ya vyandarua 1,686,933 vitakavyogawiwa katika kata 165, vijiji 656 pamoja na vituo 1,047 vya ugawaji bila malipo katika halmashauri saba za mkoa huo.

Aidha, aliwataka wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza kuacha tabia ya kuvitumia kufugia kuku au kuvulia samaki.

“Matumizi sahihi ya vyandarua ni silaha muhimu katika kutokomeza malaria, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anajilinda,” alisisitiza Malima.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3