Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MRADI WA GREEN SMART CITY SASA WAIMARISHA KILIMO CHA VIUNGO NA KUCHOCHEA UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI.

MRADI WA GREEN SMART CITY SASA WAIMARISHA KILIMO CHA VIUNGO NA KUCHOCHEA UHIFADHI WA VYANZO VYA MAJI.

 

Na Amina Saidi,Matukio Daima Media, Tanga.

Umoja wa Wakulima wa Uhifadhi wa Mazingira (UWAMAKIZI) umegawa zaidi ya miche 75,000 ya mazao ya biashara na miti ya uhifadhi kwa wakulima katika vijiji vya Shembekeza na Kwemwewe, wilayani Muheza, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuongeza kipato cha wananchi.

Miche hiyo iliyogawiwa ni pamoja na kakao zaidi ya 24,000, pilipili manga 12,000, karafuu 16,000, mdalasini 9,100 na miti ya uhifadhi aina ya kuvukuvu 8,000, Pamoja na miti ya mbao aina ya sederea 6,000 imepandwa katika maeneo mbalimbali.

Zoezi hilo linafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wa Green Smart City SASA na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA).

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa UWAMAKIZI, Twaha Mbaruku, aliwashukuru wadau kwa kufanikisha zoezi hilo na kueleza kuwa lengo ni kulinda vyanzo vya maji sambamba na kuwawezesha wakulima kiuchumi kupitia kilimo cha mazao ya biashara.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mazingira wa Tanga UWASA, Ramadhan Nyambuka, alisema taasisi hiyo inajivunia ushiriki mkubwa wa wakulima katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.


Alisema upatikanaji endelevu wa huduma ya maji katika Jiji la Tanga na miji ya Pangani, Muheza na Mkinga unategemea uhifadhi wa vyanzo vya maji katika kidakio cha Mto Zigi.


“Tunaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha juhudi za uhifadhi zinafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa jamii,” alisema Nyambuka.

Naye Mtaalamu wa Ushirikiano kutoka Taasisi ya The Nature Conservancy (TNC) na Mratibu wa Water Fund, alisema ameridhishwa na mwitikio mkubwa wa wakulima katika zoezi hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kutunza miti inayopandwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Katika hatua nyingine, ushiriki mkubwa wa vijana ulijitokeza katika zoezi hilo, ambapo walishiriki kikamilifu katika ugawaji na upandaji wa miche, hali inayotajwa kuwa chachu ya mafanikio ya miradi ya uhifadhi kwa muda mrefu.

Awali, Mtaalamu wa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Ahmed Bendera, alitoa mafunzo kwa wakulima kuhusu namna sahihi ya kupanda na kutunza miche hiyo.

Miongoni mwa wanufaika ni pamoja na  Mama Hassani alisema amenufaika na mpango huo baada ya kupokea miche 100, akieleza kuwa miche ya kakao aliyopata mwaka 2022 tayari imeanza kuzaa na kumuwezesha kupata kipato.

Alisema mpango huo umesaidia kuboresha maisha yake na kuondoa changamoto ya kipato.

Zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za makusudi za kuimarisha uhifadhi wa vyanzo vya maji huku likichochea uboreshaji wa maisha ya wananchi kupitia maendeleo ya uchumi wa kijani.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3