Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MTOTO (13) AUAWA KIKATILI IRINGA BAADA YA KUTUMWA DUKANI

MTOTO (13) AUAWA KIKATILI IRINGA BAADA YA KUTUMWA DUKANI

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA,IRINGA 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limethibitisha kifo cha kikatili cha mtoto Naomi Jostan Kivamba (13), mwanafunzi wa darasa la saba, ambaye mwili wake ulipatikana karibu na nyumbani kwao baada ya kutoweka kwa muda mfupi alipokuwa ametumwa dukani kununua kibiriti.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia, Naomi alitumwa dukani na mama yake majira ya saa sita mchana, lakini hakurejea nyumbani hali iliyowalazimu ndugu na majirani kuanza kumtafuta katika maeneo mbalimbali bila mafanikio.

Inaelezwa kuwa juhudi za kumtafuta ziliendelea hadi leo asubuhi ambapo mwili wa mtoto huyo ulipatikana kando ya nyumba yao ukiwa tayari umefariki dunia. Mwili huo ulikuwa na dalili za kufanyiwa ukatili mkubwa ikiwemo kuvunjwa mikono pamoja na kulawitiwa na watu wanaodaiwa kutekeleza tukio hilo ambao bado hawajafahamika.

Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Njia Panda alisema hilo ni tukio la pili la aina hiyo kutokea katika mtaa huo baada ya tukio lingine kama hilo kuripotiwa mwaka jana. Alitoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya dola ili kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Marehemu Naomi alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Zizi na mwaka huu alikuwa anatarajiwa kuhitimu masomo ya darasa la saba.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa  Allan Bukumbi alisema tukio hilo liliripotiwa rasmi Machi 8, 2026 majira ya saa mbili asubuhi, na askari walipofika eneo la tukio walikuta mwili wa marehemu ukiwa na majeraha ya kupigwa kwa kitu butu kabla ya kufanyiwa vitendo vya ulawiti.

Kamanda huyo alieleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini na kuwakamata wahusika waliohusika na mauaji hayo, ambapo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao mara watakapobainika.

Hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewahakikishia wananchi kuwa hali ya ulinzi na usalama mkoani humo ni shwari huku likiendelea na operesheni mbalimbali za kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu kwa lengo la kulinda usalama wa raia na mali zao.

Polisi pia imetoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahusika wa tukio hilo.



TAZAMA HAPA KUPATA MAWASILIANO YA MAJI CF

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3