MANISPAA YA BUKOBA YATAKIWA KUTOA KIPAUMBELE KWA WAFANYABIASHARA WALIOKUWA KWENYE SOKO KUU
Na Anold Deogratias Matukio Daima Media Kagera
Katibu wa NEC itikadi, uenezi na mafunzo wa chama cha mapinduzi CCM taifa Kenani Kihongosi ameitaka manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kuhakikisha wafanyabiashara waliokuwa wanafanya bishara zao katika soko kuu la Bukoba, waliondolewa ili kupisha ujenzi wa soko jipya kupewa kipaumbele pindi soko hilo litakapokamilika.
Kihongosi amesema hayo wakati alipotembelea ujenzi wa soko hilo ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ambapo ametaka wafanyabiashara hao waliokubali kupisha ujenzi wa soko kuu kupewa sehemu za kufanyia biashara zao pindi ujenzi utakaopokamilika.
"ninacho wataka manispaa ya Bukoba kuwapa kipaumbele wafanyabiashara waliokuwa wanafanya biashara zao katika soko la zamani bila upendeleo wala unafiki na kutaka kutanguliza upendo"
Aidha katika hatua nyingine Kihongosi amempongeza mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo kwa kufanya kazi kwa weledi na kasi na kutaka kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuruhusu shughuli za biashara kuendelea.
"nimpongeze mkandarasi anayetekeleza ujenzi huu, ukiangalia mradi ulianza kutekelezwa mwezi Octobar 2025 ila unaona kasi ni nzuri niwatake kukamilisha ujenzi wa soko hilo kwa muda uliopangwa ili kuruhusu shughuli za biashara kuendelea hapa"
Awali akiwasilisha taarifa za ujenzi wa soko hilo msimamizi wa mradi huo Nixon Kissa amesema mradi huo unaogharimu kiasi cha shilingi billioni 18.9 ulianza kutekelezwa tangu mwezi Octobar 2025 unatarajiwa kukamilika mwezi January 2027 na kwa sasa umefikia asilimia 19.4 za utekelezaji wake.
"mheshimiwa mgeni rasmi mradi huu ulianza kutekelezwa tangu mwezi Octobar 2025 na inatekelezwa kwa muda wa miezi 15 ambapo unatarajiwa kukamilika January 26, 2027 na inatekelezwa na mkandarasi Dimetoclasa Real Hope limited kwa ghalama ya shilingi bilioni 18.9"
Aidha msimamizi huyo amesema kuwa soko hilo litakapokamilika kutakuwa na vizimba 1848 vya kufanyia biashara maduka 234, mabucha 12 na huduma nyingine za kijamii.
Nao baadhi ya wakazi wa Bukoba akiwemo Juster Joseph amempongeza ujenzi wa soko hilo kwani ilikuwa ni hitaji la wakazi wa Bukoba kutokana na soko lililokuwepo lilikuwa chakavu na la zamani hivyo kujengwa kwa soko itakuza uchumi wa wafanyabiashara.
"nipongeze ujenzi wa soko hilo kwani itasaidia kukuza uchumi wetu wafanyabiashara kutokana na soko lililokuwepo lilikuwa chakavu na la zamani kwahiyo nipongeze serikali yetu kwa kutujengea soko jipya.
Ujenzi wa soko kuu la Bukoba ni miongoni mwa miradi minne inayotekelezwa katika manispaa ya Bukoba chini ya mradi wa kuboresha miundombinu ya ushindani wa miji Tanzania (TACTIC) pesa kutoka benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na Barabara km 10, ujenzi wa kituo cha mabasi pamoja na ujenzi wa kingo za mto Kanoni.




