MAHAFALI YA 18 KIDATO CHA SITA ST ANNE MARIE YAFANA DAR ES SALAAM
Mar 30, 2026
Na Ashrack Miraji
Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika mahafali ya 18 ya wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule za St Anne Marie Academy, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Zubeda Hassan, amepongeza uwekezaji uliofanywa na uongozi wa shule hiyo katika sekta ya elimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Zubeda alisema uwekezaji huo umeleta mageuzi chanya kwa kuboresha miundombinu ya kisasa ikiwemo majengo na maabara na maktaba zinazowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kujiandaa kuwa wataalamu mahiri watakaolitumikia taifa.
Alisema kuwa shule hiyo imeweka mfano bora wa kuigwa na taasisi nyingine za elimu nchini kutokana na ubora wa mazingira ya kujifunzia na dhamira ya dhati ya kuinua kiwango cha elimu.
“Nimetembelea maeneo mbalimbali nchini, lakini sijawahi kuona uwekezaji mkubwa kama huu katika sekta ya elimu. Niwaombe wanafunzi kuitumia vyema fursa hii kwa kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao,” alisema Zubeda.
Awali, Mkurugenzi wa Shule za St Anne Marie Academy na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, Dkt. Jasson Rweikiza, alisema mahafali hayo yamebeba mafanikio makubwa ya kitaaluma yaliyodhihirishwa na matokeo ya mitihani ya majaribio (Mock) ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema kati ya wanafunzi 190 waliofanya mitihani hiyo, zaidi ya wanafunzi 108 walipata daraja la kwanza (Division One), hatua aliyoitaja kuwa ni kiashiria cha kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya taifa inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Dkt. Rweikiza alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwepo wa walimu wenye kujituma pamoja na nidhamu ya wanafunzi, huku akisisitiza kuwa nidhamu ni msingi muhimu wa mafanikio katika maisha ya mwanafunzi.
Aidha, aliwashukuru wazazi kwa kuendelea kuiamini shule hiyo na kusisitiza kuwa ushirikiano mzuri kati ya walimu na wazazi unaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza maendeleo ya kitaaluma na kitabia kwa wanafunzi.



