Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
EID EL-FITR: WAISLAMU DUMISHENI MAADILI MEMA-SHEKHE MKOA SINGIDA

EID EL-FITR: WAISLAMU DUMISHENI MAADILI MEMA-SHEKHE MKOA SINGIDA

 


‎Na Elisante John, Singida

‎Shekhe wa Mkoa wa Singida, Alhaji Issah Nassoro, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu na jamii nzima ya Tanzania, kuhakikisha inadumisha maadili mema, kuimarisha ndoa na umoja baina yao, ili kuharakiaha maendeleo ya familia, na Taifa kwa ujumla.

‎Akiongoza waumini wa Kiislamu kwenye  Ibada ya Eid kimkoa, iliyofanyika kwenye uwanja wa Bombadia mjini Singida, Alhaji Shekhe Nassoro amesema changamoto nyingi zinazoikumba jamii ya Kiislamu, hasa ongezeko la talaka, ni waumini wake kupuuza mafundisho ya mwenyezi Mungu na tamaa ya wanawake kupata mali.

"Kwa sasa talaka zimefikia 1,000, jambo ambalo linachochea ongezeko la watoto wa mitaani, na hali hii inahitaji mabadiliko ya haraka," alisema Alhaji Shekhe Nassoro.


‎Alisema waumini wa Kiislamu wanapaswa kuvumiliana na kuwa na tabia nzuri, ili kuepuka migongano na mivutano, inayochangia wanandoa kupeana talaka hata kwa jambo dogo linalohitaji suluhu, badala yake ndoa inavunjika, kurokana tu na wanawake baadhi kutaka kujikomboa kiuchumi, jambo ambalo linavuruga familia nyingi.

Alhaji Shekhe Nassoro aliwahimiza waumini wa Kiislamu kuzingatia misingi ya Kiislamu katika ndoa zao, akisema kuwa kila mume na mke wanapaswa kumheshimu mwingine na kuishi kwa upendo na umoja. "Taarifa inaoyesha ndoa 500 zilizovunjika, ni dhahiri dalili zote ni kushindwa kwa baadhi ya wanandoa kutii misingi ya ndoa iliyowekwa na mwenyezi Mungu...Tuache kuzichezea ndoa zetu, kuimarisha ndoa ni jukumu la kila mmoja katika familia, na usuluhishi kabla ya talaka kutolewa inapaswa kuwa ni suala la kipaumbele," alisisitiza alhaji shekhe Nassoro.

‎Kuhusu Mipango ya Maendeleo ya Afya kwa Bakwata, Alhaji Shekhe Nassoro amesema mkoa unatarajia hivi karibuni kuanza ujenzinwa vituo vya afya na chuo cha wataalamu wa tiba, wakiwemo madaktari na wauguzi, ili kuboresha huduma za afya kwa jamii.

Alieleza Moja ya mkakati uliopo ni kuwa katika wilaya ya Manyoni, tayari Bakwata  imepata ekari 100 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho, huku mabweni manane yakiwa tayari yameshajengwa.

‎Alhaji shekhe Nassoro alitumia fursa hiyo kuwahimiza waumini wote na wadau wengine wa maendeleo, kuchangamkia fursa hiyo kwa kuchangia fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya afya, ili jamii ya Kiislamu iweze kunufaika na huduma bora zaidi.

‎Kwa upande wake Suleimani Mwenda, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego, aliomba waumini hao kudumisha amani, kuwa na familia bora, na kushiriki katika shughuli zote za maendeleo. 

"Umoja wa familia ni muhimu katika kupunguza uhalifu na kuleta maendeleo, kadhalika malezi bora katika familia ni jambo muhimu sana kwa ustawi wa jamii," alisema Mwenda, huku pia kitoa wito kwa waumini hao kushirikiana kujikita katika shughuli za biashara, kilimo, na uvuvi ili kuimarisha uchumi wao, mkoa na Taifa kwa ujumla.


Wakitoa maoni yao kuhusu hali ya ndoa mkoani Singida, baadhi ya waumini akiwemo Ziana Said Salumu, alisema kuwa ndoa nyingi zinavunjika kutokana na sababu nyingi, ikiwemo wanawake kujikita katika kutafuta mali, huku wakipuuza majukumu yao ya kifamilia.


 "Wanawake wengi wameacha kuheshimu waume zao, na kupuuza misingi ya Kiislamu...hali hii inahitaji mabadiliko, na nawahimiza wanawake na wanaume, warejee katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu ili kuimarisha familia zao," alisema.

‎Mwisho Waumini walikubaliana na wito wa Shekhe Nassoro na mgeni rasmi, kwa kuchangia fedha za ujenzi wa kituo cha afya Manga, na chuo cha Tiba Manyoni, na fedha Taslimu zaidi ya Sh. 20,000,000/zikichangwa, na ramani ya kituo cha Afya Manga kitakachogharimu Sh. milioni 500, ikikabidhiwa. Kati ya fedha hizo Milioni Kumi zimetolewa na Bakwata na kiasi kingine ofisi ya mkuu wa mkoa Singida, kwa kushirikiana na wilaya zake Tano.

‎MWISHO.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3