BALOZI LUVUNDA -TANZANIA IONGEZE KASI KUINGIA SOKO LA KIMATAIFA LA KABONI
Na Matukio Daima, Morogoro
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira ) Balozi Baraka Luvanda amekitaka Kituo cha Taifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kuongeza juhudi za kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika masoko ya kimataifa ya biashara ya kaboni.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza kikazi katika kituo hicho tangu kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Luvanda alisema ni muhimu kuimarisha miradi ya kaboni inayohusisha sekta mbalimbali ikiwemo misitu, uchumi wa buluu na nishati mbadala ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa taifa.
Alisema biashara ya kaboni ni moja ya maeneo yanayokua duniani na Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika ikiwa itaendelea kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira pamoja na miradi ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kufuatilia Kaboni, Kathryn Kigaraba, alisema kituo hicho kitaendelea kusimamia ufuatiliaji wa gesi joto pamoja na kuratibu biashara ya kaboni ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na fursa za kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa kituo hicho kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 ikiwa ni taasisi ya kimkakati ya kitaifa inayoratibu shughuli zote zinazohusiana na biashara ya kaboni nchini.


