FCC YARIDHIA UNUNUZI WA MAKAMPUNI YA KILIMO YENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 20.4
Na Hamida Ramadhan, matukio Daima Media Dodoma
TUME ya Ushindani (FCC) imeridhia ununuzi wa makampuni mawili katika sekta ya kilimo wenye thamani ya jumla ya Shilingi bilioni 20.4 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26, hatua inayolenga kuimarisha uwekezaji, kuongeza mitaji na kupanua wigo wa masoko kwa makampuni hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5, 2026, katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, amesema uamuzi huo pia unalenga kusaidia makampuni hayo kuendelea kufanya shughuli zake bila kukabiliwa na hatari ya kuondoka sokoni.
Amesema moja ya makampuni yaliyopata kibali cha ununuzi ni Africado Limited, kampuni inayojishughulisha na uzalishaji na usafirishaji wa maparachichi katika masoko ya kimataifa, ambayo imenunuliwa na kampuni ya uwekezaji ya AgDevCo Limited kwa kushirikiana na Bw. Garth John Weston.
Kwa mujibu wa Ngasongwa, AgDevCo ni kampuni ya uwekezaji inayotoa mikopo na mitaji kwa biashara changa za kilimo katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ameeleza kuwa muungano huo unatarajiwa kuchochea ukuaji wa shughuli za Africado Limited kwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa kibiashara pamoja na kuimarisha ushirikiano na wakulima wadogo.
“Hatua hii itasaidia pia wakulima wadogo kunufaika kupitia huduma za ugani pamoja na upatikanaji wa masoko ya kimataifa kwa mazao yao,” alisema.
Katika hatua nyingine, amesema FCC pia imeridhia ununuzi wa kampuni ya Amboni Spinning Mill Limited na kampuni ya Amboni Sisal Properties Limited (ASPL).
Amesema kampuni ya Amboni Spinning Mill Limited inamiliki kiwanda kilichopo mkoani Tanga kinachojishughulisha na uchakataji na usindikaji wa zao la katani pamoja na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo nyuzi na kamba.
Ngasongwa amebainisha kuwa muungano huo unatarajiwa kuongeza uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa zao la katani kuanzia uzalishaji, usindikaji hadi uuzaji wa bidhaa zake.
Ameongeza kuwa FCC itaendelea kusimamia miungano ya biashara ili kuhakikisha inaleta tija katika uchumi wa nchi huku ikiimarisha ushindani wa haki sokoni.




