WANAHABARI WAPEWA MAFUNZO YA UCHUNGUZI WA MAZINGIRA
Na Pamela Mollel, Arusha
Wanahabari nchini wametakiwa kutumia kalamu zao kama chombo cha mabadiliko katika kulinda mazingira na kutetea haki za jamii, kufuatia kuongezeka kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyoathiri maisha ya wananchi, uchumi na mustakabali wa rasilimali asilia kitaifa na kimataifa.
Wito huo umetolewa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Asili (MAIPAC) wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi wa mazingira kwa wanahabari wa Kanda ya Kaskazini na Kati, yanayofanyika jijini Arusha kuanzia Februari 5, 2026.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wanahabari 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Singida na Dodoma, yakilenga kuwajengea uwezo wa kuchunguza, kuandika na kuripoti kwa kina masuala ya mazingira yanayoigusa jamii moja kwa moja. Programu hiyo inafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Programu na Uendeshaji wa THRDC, Wakili Halima Sonda, amesema wanahabari wana nafasi muhimu katika kuhabarisha umma kuhusu athari za uharibifu wa mazingira ikiwemo uchafuzi wa mazingira, ukataji miti hovyo, uchimbaji holela wa madini pamoja na matumizi yasiyo endelevu ya ardhi.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wanakusudia kuwajengea uwezo wanahabari ili waweze kuandika habari za uchunguzi zenye ushahidi, zitakazosaidia kuelimisha jamii, kuwawajibisha wahusika na kuchochea hatua madhubuti za uhifadhi wa mazingira.
Naye Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma, ameeleza kuwa uandishi wa habari za mazingira una mchango mkubwa katika kulinda haki za binadamu, hususan kwa jamii za asili zinazotegemea rasilimali za mazingira kwa maisha na utamaduni wao.
Ameongeza kuwa taasisi hizo zinatarajia kuwafikia wanahabari 140 nchi nzima kupitia mafunzo hayo, yatakayogusa pia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa taka ngumu, uhifadhi wa wanyamapori pamoja na matumizi endelevu ya ardhi.
Kwa upande wake, Wakili Paulo Kisabo aliyetoa mada kuhusu sheria za ardhi, mazingira na habari, amesisitiza wanahabari kuzingatia misingi ya kisheria wanapotekeleza majukumu yao, akibainisha kuwa sheria nyingi zinawalinda wanapofanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma.
Mafunzo hayo yanaendelea jijini Arusha huku yakitarajiwa kufanyika pia katika kanda nyingine nchini, yakilenga kuongeza idadi ya wanahabari wenye ujuzi wa kuandika na kuchunguza masuala ya mazingira ili kuimarisha uhifadhi na maendeleo endelevu ya taifa


