AJERUHIWA KWA RISASI NA KUPORWA FEDHA AKITOKA BENKI.
Na Josea Sinkala, Songwe.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Augustino Senga, amesema mtu mmoja mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, amejeruhiwa baada ya kufuatuliwa risasi na watu wasiojulikana wakati akitoka benki kisha kumpora fedha.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, amesema tukio hilo la uhalifu lililotokea tarehe 04 Februari, 2026 majira ya saa nne asubuhi, katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga Tunduma, Wlwilaya ya Momba mkoani wa Songwe.
Amesema katika tukio hilo, mtu aitwaye Yengo Mwapina Mkazi wa Sogea Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, alishambuliwa na watu watatu wasiojulikana akiwa njiani kutoka Benki mjini Tunduma ndipo washambuliaji hao walimfyatulia risasi na kumsababishia jeraha kiunoni upande wa kushoto na kumnyang’anya fedha taslimu kiasi cha Shilingi Milioni Hamsini na Nne (54,000,000) za Kitanzania.
Ameeleza kuwa majeruhi huyo alikimbizwa katika kituo cha Afya Tunduma alipopatiwa matibabu ya awali na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe, linaendelea na uchunguzi wa kina sambamba na msako ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa tukio hilo na kuwafikisha Mahakamani.
Katika tukio lingine Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa taarifa ya tukio la kifo kilichotokea tarehe 01 Februari, 2026 saa saba mchana katika maeneo ya mto Itemba, kijiji cha Lukululu, kata ya Mlangali, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, tukio lililomhusisha Feriki Kareai (54) Mkulima, Mkazi wa Kijiji cha Lukululu Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, alikutwa akiwa amefariki Dunia huku mwili wake ukiwa umefukiwa na kifusi pembeni mwa Mto Itemba.
Polisi imkupitia kamanda Senga inasema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo, marehemu alikuwa anachimba kifusi hicho kwa lengo la kutafuta madini aina ya dhahabu, hali iliyopelekea kifusi hicho kuporomoka na kumfukia na kusababisha kifo chake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini kiholela na bila kufuata taratibu za usalama.
