WANACHAMA CCM NA WANANCHI MWANZA. WATAKIWA KULINDA AMANI NA UMOJA
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Katika kusherehekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanachama na wananchi wa Mkoa wa Mwanza wametakiwa kuchukua jukumu la kulinda na kudumisha Amani, Umoja, na Mshikamano katika nyanja zote za maisha.
Hayo yamebainishwa leo, Februari 5, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, katika sherehe zilizofanyika Jimbo la Sumve, Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza.
Mongella, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimejenga misingi imara ya Amani, Umoja, na Mshikamano, ambazo ndizo zilizozaa maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa nchini Tanzania.
"Amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yetu. Bila amani, hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana," alisema Mongella, akisisitiza kuwa misingi hiyo imara ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa letu.
Aidha, alielezea kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatimiza miaka 49 kikiwa kimejizatiti katika masuala ya misingi ya Amani, Umoja, na Mshikamano, na hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya ustawi wa Taifa.
Mongella ameeleza kuwa licha ya changamoto mbalimbali, CCM itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Amani na Umoja vinadumishwa ili kuleta maendeleo endelevu.
Kwa upande mwingine, Mongella alitoa pongezi kwa viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Mwanza kwa usimamizi madhubuti na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya sita ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo yaliadhimishwa kwa kauli mbiu isemayo “Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Taifa letu,” ikiwa ni ishara ya kuendelea kudumisha misingi hiyo muhimu kwa manufaa ya wananchi wote.




