MTOTO ALIWA NA MAMBA AKIOGA MTO SIMIYU.
Na COSTANTINE MATHIAS, Matukio Daima-Simiyu.
MTOTO aliyefahamika kwa jila la Paul Petro (14), mkazi wa kijiji cha Malita wilayani Maswa mkoani Simiyu amefariki dunia baada ya kushambuliwa na Mamba wakati anaoga na wenzake wawili katika mto Simiyu, majira ya saa moja jioni siku ya February 4, mwaka huu.
Mtoto huyo aliambatana na wenzie wawili ambao ni manusura mmoja akifahamika kwa jina moja la Baraka na Emmanuel Paul walifika katika mto huo baada ya kutoka kucheza mpira ikiwa ni desturi ya wanakijiji wa kijiji hicho kutumia maji ya mto huo kwa matumizi mbalimbali ikiwepo kuoga, kufulia na kunywesha mifugo.
Akielezea tukio hilo Emmanuel Paul mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Zanzui ambaye ndiye alitoa wazo la yeye na wenzie kwenda kuoga anasema kuwa baada ya kuona hali iliyomstua alioamua kuwaambia wenzie watoke mtoni kabla ya mamba kumvuta Paul.
“Nilipotoka shule nilirudi nyumbani na kuchukua kinyavu na dodoki nikaelekea mtoni ila kabla sijafika nikawakuta wenzangu Baraka na Paul wanacheza mpira nikaanza kucheza kisha nikawaambia tuelekee mtoni kuoga,” amesema Emmanuel.
“Mimi nilioga sehemu ya kina kifupi wenzangu walikuwa ndani ya maji na nikaona kitu ambacho sikukielewa nikatoka haraka kuwaambia wenzangu watoke sasa wakati Paul ametoka akapigwa na mkia wa mamba mguuni akaanza kulia akiwa hapo mamba akaibuka mkubwa akamvuta mgongoni na kuondoka nae hapo ndipo Baraka nae akatoka haraka kwenye maji,...nikachanganikiwa ila kuna mama alikuja hapo akaniambia niende kwao kuwaambia Paul kabebwa na mamba,” anasema Emmanuel.
Akithibitisha tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Musa Maige amesema kuwa majira ya saa moja jioni alipokea simu kutoka kwa wananchi wakimueleza tukio hilo ndiyo alipoamua kuitisha mwano ili watu wakusanyika kujua ni hatua zipi zianze kuchukuliwa kumtafuta mtoto huyo.
“baada ya simu niliitisha mwano tukusanyike wanakijiji ili tushuhudie na tune namna ya kumtafuta, tulianza kumtafuta siku ile hatukumuona tukakubaliana alfajiri ya leo saa 9 tuanze kazi kwa hiyo tumekuwa hapa hadi jioni hii kumpata mtoto,” amesema Mwenyekiti huyo.
Ameongeza kuwa alifanikiwa kutoa taarifa jeshi la polisi pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya baada ya kuona msaada unachelewa waliamua kufanya wenyewe jitihada zote.
Hata hivyo amekiri kuwa mto huo umekuwa ukitumiwa siku zote kutokana na uhaba wa maji uliopo kijijini hapo licha ya kutambua uwepo wa mamba zaidi ya thelathini waliowatolea taarifa kwa ofisi ya maliasili ili waje kuwatoa zoezi ambalo bado halijatekelezwa.
Emmanuel Mabula mjomba wa marehemu anasema kuwa mtoto huyo hupendelea kuishi na bibi yake katika kijiji hicho kwani wazazi wake wanaishi kijiji cha karibu cha Mwamalapa.
“huwa anakaa na bibi yake mara nyingi anachunga ng’ombe wazazi wake hawapo hapa na hii taarifa inanifikia nilikuwa jijini Mwanza ndiyo nikawahi kuja huku kuendelea na jitihada za kumtafuta, kipekee nishukuru ushirikiano wa wananzengo kuanzia alfajiri hadi sasa kumpata,” anasema Emmanuel Mabula mjomba wa marehemu.
Baada ya mwili kupatikana majira ya saa kumi na nusu jioni umepelekwa kwatika hospitali ya wilaya ya Maswa na baada ya maandalisi kukamilika Paul anatarajiwa kuzikwa February 6, 2026 katika kijiji cha Malita.
Mwisho.


