UGENI WA WAKALA WA NGUVU ZA ATOMIKI DUNIANI (IAEA) KUTEMBELEA KITUO CHA TAEC ARUSHA, KUKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI
Na Pamela Mollel,Arusha
Ugeni kutoka Wakala wa Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) umetembelea kituo cha Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) kilichopo Arusha. Ziara hii inalenga kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na wakala huo, sambamba na kutathmini maendeleo yake na uwezekano wa ufadhili endelevu..
Katika ziara hiyo, La Cashaw Wolde na Bw. Keshan Azza, viongozi kutoka IAEA wenye makao yake Austria, wakiwa katika programu ya Africa Programme, walikutana na viongozi wa TAEC. Wameangalia miradi ikiwemo uboreshaji wa mbegu bora kwa kutumia teknolojia ya nyuklia, ujenzi wa maabara ya kisasa, na mradi wa irradiator unaolenga kuhifadhi na kuongeza ubora wa mazao.
Pia, ugeni huu umeangalia mradi mkubwa wa kuongeza vituo vya matibabu ya saratani nchini kutoka vinne hadi kufikia sita, mradi unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi na kupunguza mzigo kwenye vituo vya sasa.
Kwa mujibu wa TAEC, ziara hiyo inalenga kuwezesha IAEA kutoa ufadhili na msaada wa kitaalamu zaidi, sambamba na kuimarisha ushirikiano katika matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo ya kilimo, afya na sayansi nchini Tanzania.
Uongozi wa TAEC umeeleza kuwa miradi hii ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kutumia sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa maendeleo endelevu, huku ukisisitiza kuwa ushirikiano na IAEA umeleta manufaa makubwa kwa wananchi kupitia ongezeko la uzalishaji wa chakula na kuboreshwa kwa huduma za matibabu ya saratani.

