Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
VIJANA LINDI WAJITOKEZA KUOMBA BILIONI 2 ZA MAKONDA

VIJANA LINDI WAJITOKEZA KUOMBA BILIONI 2 ZA MAKONDA

 


NA MATUKIO DAIMA MEDIA ,LINDI 

Baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda kutangaza kuwa Serikali imetenga TZS bilioni 2 kwa ajili ya kuwawezesha watengenezaji wa maudhui mtandaoni, vijana wa Manispaa ya Lindi wamejitokeza kwa wingi katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kupitia Kitengo cha Habari kujisajili na kuchukua fomu za maombi.


Fedha hizo zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuyawezesha makundi ya watengenezaji wa maudhui katika sekta mbalimbali zikiwemo utalii, michezo, habari, jamii, muziki, filamu na sanaa nyinginezo. Mpango huo unalenga kukuza ajira kwa vijana pamoja na kuimarisha uchumi wa kidijitali nchini.


Akizungumza ofisini kwake, Afisa Habari wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Ndg. Daula Moony, amesema mwitikio wa vijana umekuwa mkubwa tangu kuanza kwa zoezi hilo Januari 30, 2026.

“Vijana wa Lindi wameonesha utayari mkubwa wa kuchangamkia fursa hii ya bilioni 2. Hii ni nafasi ya kipekee kwao kuendeleza vipaji vyao na kujiongezea kipato kupitia majukwaa ya kidijitali,” amesema Daula.

Ameongeza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea hadi Februari 15, 2026, na amewahimiza waombaji kuhakikisha wanajaza fomu kwa usahihi pamoja na kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu kazi wanazozifanya.

“Tunataka kuona maudhui yenye ubunifu, yenye maadili na yanayotangaza fursa na vivutio vya Lindi kwa manufaa ya jamii,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Asia Ahamadi, mmoja wa watengenezaji wa maudhui aliyefika kuchukua fomu, amesema fursa hiyo imeleta matumaini mapya kwa vijana wa mkoa huo.

“Serikali imetuamini na kututhamini. Sasa ni jukumu letu kuonyesha uwezo wetu. Tukipata uwezeshaji huu, tutaboresha vifaa, kuongeza ubora wa kazi na kuitangaza Lindi kitaifa na kimataifa,” amesema Asia.

Mwitikio huo unaonesha dhamira ya vijana wa Manispaa ya Lindi kutumia teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya kujiletea maendeleo, huku fursa ya bilioni 2 ikitajwa kuwa chachu ya kukuza ajira na uchumi wa kidijitali katika eneo hilo.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3