MWIGULU NCHEMBA KUPAMBA MAADHIMISHO YA CCM KIGOMA
Katibu wa siasa, uenezi na mafunzo CCM mkoa Kigoma Deogratius Nsokolo akizungumza na waandishi wa habari akieleza ratiba ya maadhimisho ya sherehe za miaka 49 ya kuzaliwa CCM kwa ngazi ya mkoa Kigoma ambapo Waziri Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba anatarajia kuhitimisha kilele cha sherehe hizo mkoani Kigoma.
(Picha na Fadhili Abdallah)
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Dk.Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 49 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kigoma Februari tano mwaka huu ambapo suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi itakuwa ajenda ya maadhimisho hayo.
Katibu wa siasa, uenezi na mafunzo CCM mkoa Kigoma, Deogratius Nsokolo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari alisema kuwa Mwigulu ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa mkoa Kigoma atahitimisha maadhimisho hayo katika sherehe zitakazo fanyika uwanja wa Kiganamo wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Nsokolo alisema kuwa uzinduzi wa maadhimisho hayo utafanyika jumatatu Februari mbili katika viwanja vya Kwa Noti Ujiji mkoani Kigoma ambapo Mwenyekiti wa CCM mkoa Kigoma Jamal Tamim anatarajia kuzindua maadhimisho ya sherehe hizo.
Sambamba na hilo Nsokolo alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu kwa mkoa Kigoma suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira itakuwa ni ajenda ya maadhimisho hayo ambapo wanatarajia kupanda miti Zaidi ya 10,000 huku matumizi ya nishati safi itakuwa pia ajenda itakayozungumzwa kwenye mikutano na ratiba mbalimbali zitakazopangwa.
Aidha Katibu Mwenezi huyo wa CCM mkoa Kigoma alisema kuwa maadhimisho hayo pia yataenda sambamba na Kamati ya siasa ya mkoa Kigoma kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na mamlaka za serikali ikiwa ni kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.
