Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MONGELA, DKT, SAMIA DHAMIRA YAKE NI KUBORESHA SEKTA YA AFYA

MONGELA, DKT, SAMIA DHAMIRA YAKE NI KUBORESHA SEKTA YA AFYA


NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA MWANZA.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), John Mongela, ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka dhamira thabiti katika sekta ya afya kuhakikisha inaimarika na kuleta ustawi kwa jamii.

Hayo ameyabainisha leo, Februari 4, 2026, alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 49 ya chama hicho na kueleza  kuwa jamii yenye afya njema inaweza kushiriki vyema katika shughuli za maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

"Jamii ambayo inapata elimu bora ndiyo jamii inayoweza kupambana na changamoto za kisasa. Tunaona kuna miundombinu ya kila aina hapa Mwanza, na maboresho makubwa yamefanyika hasa katika sekta ya afya," Alisema Mongela.


Aidha, Mongela amefafanua kuwa katika kipindi cha siku mia moja za utawala wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya afya imeanzisha bima ya afya itakayogusa kila Mtanzania kwa nafasi yake.

"Kuna baadhi ya Nchi ambazo hazijafika katika ngazi hii Sisi ambayo  tumefika hapa, katika siku mia moja za kipindi Cha awamu ya sita," Alisema Mongela.


Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure, Dkt. Bahati Msaki, ameeleza kuwa hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wa nje kati ya 450 hadi 500 kwa siku, na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 60 kwa siku.

Aidha, Dkt. Msaki alieleza kuwa hospitali hiyo ilipokea mashine ya CT-Scan kutoka Wizara ya Afya kupitia mradi wa usambazaji vifaa tiba vya mionzi (ORIO), yenye thamani ya bilioni mbili.

"Uwepo wa mashine hii umeboresha huduma mbalimbali za uchunguzi ambapo kuanzia julai,2025 hadi Disemba 2025 jumla ya wagonjwa 934 wamepatiwa huduma za uchunguzi, na imepunguza idadi ya wagonjwa ambao walikuwa wanapewa rufaa kwenda kufanya kipimo katika Hosptali ya Kanda ya Bugando", Amesema Dkt. Msaki

Pia, Dkt. Msaki alifafanua kuwa hospitali hiyo ina mashine kumi za kutoa huduma ya kusafisha damu (Dialysis), huduma ambayo ilianza kutolewa Machi 2022, ambapo wagonjwa 101 wamenufaika na huduma hiyo, na 11 wanaendelea na huduma hadi sasa.

Akizungumzia maboresho yanayoendelea Dkt. Msaki amesema kuwa hospitali hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa jengo jipya la kisasa lenye thamani ya bilioni 22 ambapo Jengo hilo litakuwa na ghorofa tisa na litahudumia wagonjwa wa dharura na ajali (EMD), OPD, na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

"Wizara ipo kwenye mpango wa kumtafuta mkandarasi kwa mwaka 2022/2023. Hospitali iliingiziwa bilioni moja, na hivi sasa Wizara ya Afya inakamilisha taratibu za kumpata mkandarasi, kwani mshauri mwelekezi tayari ameshapatikana," alisema Dkt. Msaki.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3