Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BODABODA IRINGA WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA VYAMA ILI KUNUFAIKA NA MIKOPO

BODABODA IRINGA WAHAMASISHWA KUJIUNGA NA VYAMA ILI KUNUFAIKA NA MIKOPO

Mwenyekiti wa umoja wa bodaboda Mkoa wa Iringa Zuberi Mapila (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kipindi cha Tanzania ya leo Matukio Daima Media wakati akihojiwa na mwendeshaji wa kipindi hicho  Francis Godwin,Picha na Matukio Daima Media

NA BERDINA MAJINGE MATUKIO DAIMA MEDIA

Madereva wa bodaboda mkoani Iringa ambao bado hawajajiunga na chama cha bodaboda wamehimizwa kujiunga ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo mikopo ya halmashauri pamoja na mafunzo ya usalama barabarani.

Akizungumza katika kipindi cha Tanzania ya Leo kinachorushwa na Matukio Daima Media, Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Iringa, Zuberi Mapila, alisema kuwa uanachama wa chama hicho unamwezesha dereva kupata elimu ya usalama barabarani, mikopo nafuu na fursa nyingine za kiuchumi.

Mapila alisema kuwa ni nafuu zaidi kwa dereva wa bodaboda kupata mkopo kutoka halmashauri kwa ajili ya kununua pikipiki kuliko kukopeshwa bodaboda kwa mfumo wa mikataba kutoka kwa watu binafsi, ambao mara nyingi huwa na masharti magumu.

Alifafanua kuwa hadi sasa Mkoa wa Iringa una zaidi ya bodaboda 10,000 zilizopatikana kupitia mikopo ya halmashauri, huku ofisi ya chama cha bodaboda mkoani humo ikiwa na zaidi ya pikipiki 15 walizozipata kupitia mkopo wa asilimia 10.

“Dereva anayekopeshwa bodaboda anatakiwa kuhakikisha anarejesha marejesho kwa uaminifu na kwa wakati ili kujenga sifa ya chama na kuhakikisha kazi ya bodaboda inaendelea kuheshimika. Tumekuwa na changamoto ambapo vijana wengi huingia mikataba, lakini wanapokaribia kumaliza marejesho hudai kuwa bodaboda zimeibiwa. Hili ni jambo linalohitaji umakini mkubwa,” alisema Mapila.

Aidha, alisema kuwa vijana wote wanaotaka kujiingiza katika kazi ya bodaboda wanapaswa kufika katika ofisi za chama kwa ajili ya kupata elimu sahihi, badala ya kujifunza katika vituo vya bodaboda, akisisitiza kuwa ofisi za chama ni salama zaidi.

Mapila pia alisema kuwa chama kimezungumza na baadhi ya benki na kukubaliana kuwa badala ya kutoa fedha taslimu, wakopaji wapewe bodaboda moja kwa moja ili kurahisisha urejeshaji wa mikopo hiyo.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa madereva wa bodaboda wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kuacha mara moja, akisema vitendo hivyo havikubaliki katika jamii na vinachafua taswira ya sekta hiyo.

TAZAMA FULL MAHOJIANO BOFYA LINK HII

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3