SERIKALI KUANZISHA MFUKO WA KITAIFA KUWEZESHA KAMPUNI CHANGA ZA TEHAMA
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
SERIKALI , kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeanza maandalizi ya kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA (ICT Startups Development Fund), ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za siku 100 za uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumzia mpango huo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angela Kairuki, amesema mfuko huo utalenga kuwawezesha vijana wabunifu kupata mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara zao.
"Tunalenga kukuza biashara zao hususan kampuni changa ambazo mara nyingi hazipati mikopo kutoka benki na taasisi nyingine za fedha, " Amesema
Waziri Kairuki amefafanua kwamba mfuko huo utawasaidia vijana kuboresha bidhaa na huduma wanazotoa, kuongeza ushindani sokoni na kufikia masoko kwa haraka zaidi, hatua itakayochochea ukuaji wa sekta ya TEHAMA na kuongeza ajira kwa vijana nchini.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana wabunifu ili bunifu zao ziwe na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali na ustawi wa taifa kwa ujumla.

