MKANDARASI WA SKIMU YA UMWAGILIAJI MKOMBOZI APEWA SIKU MBILI KUKAMILISHA MRADI
sehemu ya Skimu ya umwagiliaji mradi wa Mkombozi ambayo haijakamilika
Na Catherin Kilwale (UoI), Matukio Daima Media
Wananchi wa kijiji cha Mbugani, kata ya Mboliboli wilaya ya Iringa wanaojishughulisha na kilimo cha zao la mpunga kupitia Skimu ya umwagiliaji Mradi wa Mkombozi, wamempa mkandarasi wa mradi huo siku mbili kuhakikisha kuwa mradi unakamilika na kuanza kutumika.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, wananchi na wakulima wa mpunga walieleza malalamiko yao mbele ya Diwani wa Kata ya Mboliboli pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo, wakidai ucheleweshaji wa mradi unasababisha kupotea kwa msimu wa kilimo.
Mmoja wa wananchi alisema kuwa chanzo kikuu cha tatizo hilo ni usimamizi dhaifu wa mkandarasi mkuu kwa wakandarasi wadogo.
“Adui yetu kwenye mradi huu ni mkandarasi, kwa sababu ameshindwa kuwasimamia wakandarasi wadogo Msimu wa kilimo unapita kwa sababu yake. Kama angekuwa anawasimamia vizuri, changamoto hizi zisingekuwepo inabidi abakie hapa mpaka mradi ukamilike,” alisema mwananchi huyo kwa hasira.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mboliboli, Yusuphu Msamba, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali imepokea malalamiko yao na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya siku mbili.
“Malalamiko tumeyapokea na tunatarajia kuanzia kesho mradi uanze kufanya kazi. Mkandarasi yupo hapa na amesikia changamoto zote,” alisema Msamba.
Aidha, diwani huyo alimshauri mkandarasi kuongeza njia ya maji kutoka TC13 hadi TC16 ili kuelekeza maji katika maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa, akisema bila kufanya hivyo changamoto ya upatikanaji wa maji itaendelea kuwepo.
Msamba pia aliwataka wananchi na wakulima kuendelea kuwa na subira huku akisisitiza umuhimu wa mkandarasi kupokea na kufanyia kazi ushauri unaotolewa na wananchi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza baadaye.
Naye Mkandarasi Mkuu wa Mradi wa Umwagiliaji Mkombozi, Peter Akonai, aliwaahidi wananchi kuwa atafanya tathmini ya kina ili kubaini na kurekebisha changamoto zilizopo, ikiwemo chujio zilizoharibika na kusababisha ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo.
“Ninawaondoa hofu wakulima na ninawahakikishia kuwa nitaweka kambi pamoja na wakandarasi wadogo kuhakikisha kila eneo linapata maji ya kutosha. Nitahakikisha marekebisho yanafanyika ndani ya siku mbili,” alisema Akonai
Mradi huu wa unajengwa na kampuni ya COMFIX AND Engineering Company na CRJE Chinese EAST Africa Company,mradi huu wa Mkombozi unanufaisha kata mbili za Mboliboli na Itunundu ambapo walengwa zaidi 20,000 watanufaika,mradi huu asilimia 80 upo kata Mboliboli na asilimia 20 upo kata ya Itunundu na una jumla ya Hekari 15,0000 utajengwa kwa Tsh Bilioni 56 fedha kutoka Serikaki kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji



