Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
DC SITTA AWAHIMIZA WANUFAIKA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KUREJESHA KWA WAKATI

DC SITTA AWAHIMIZA WANUFAIKA MIKOPO YA ASILIMIA 10 KUREJESHA KWA WAKATI

 

Na Emmanuel Manonga Matukio Daima Media -0754026299 

Mkuu wa Wilaya ya Iringa mkoani Iringa  Benjamin Sitta, amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kurejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika, sambamba na kujijengea sifa ya kupata mikopo mikubwa zaidi kutoka taasisi za kifedha.

Sitta alitoa wito huo leo Februari 10, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya Gangilonga, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa.


Katika hafla hiyo, jumla ya shilingi 479,517,300 zilitolewa kwa vikundi 40, ambapo vikundi 26 ni vya wanawake, vikundi 9 vya vijana na vikundi 5 vya watu wenye ulemavu.

Alisema kuwa bado kuna vikundi 30 vyenye jumla ya watu takribani 150 ambavyo havikupata mikopo hiyo kutokana na kutokidhi vigezo, huku akisisitiza kuwa vikundi vilivyopata fedha hizo vimebahatika kukutana na fursa kwa wakati muafaka.

“Fursa hii na wakati huu unaweza usijirudie tena au unaweza kujirudia, lakini hilo litategemea namna mtakavyotumia fedha hizi. Zitumikeni kwa nidhamu na malengo,” alisema Bw. Sitta.

Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kuwawezesha wananchi kiuchumi ili kujikwamua kutoka kwenye umaskini, akibainisha kuwa mikopo hiyo haina riba lakini inapaswa kurejeshwa kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wengine walioko kwenye orodha ya kusubiri.

Bw. Sitta pia aliwakumbusha wanufaika kuwa changamoto ni sehemu ya safari ya maendeleo, akitolea mfano gharama za harusi au matibabu ambazo zinaweza kuwafanya baadhi ya watu kutumia vibaya fedha za mikopo.


“Fedha hizi zinahitaji nidhamu kubwa. Hata wafanyabiashara wakubwa wakati mwingine hufeli, hivyo mjipange vizuri ili msije mkapata shida pindi marejesho yatakapohitajika,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bi. Zaina Mlawa, aliwataka wanufaika kuhakikisha wanajiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwao na familia zao.

“Serikali imezindua mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo mchango ni shilingi laki moja kwa familia ya watu sita, ikiwemo baba, mama na wategemezi wanne. Kupitia uwekezaji wa mikopo hii mtapata uwezo wa kumudu gharama hizo,” alisema Bi. Mlawa.


Aidha, alieleza kuwa kuanzia Julai hadi Februari, Manispaa ya Iringa imekuwa ikitekeleza sera ya kutenga asilimia 30 ya manunuzi yake kwa makundi maalum, sambamba na kutoa ufuatiliaji na usaidizi kwa vikundi ili kuviwezesha kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Gaudensi Nombo, kijana mnufaika wa mkopo huo, alisema kuwa wao kama wanufaika wamejipanga vizuri kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili waweze kukopa tena kwa viwango vikubwa zaidi.

“Tumejipanga kurejesha mikopo hii kwa wakati ili sisi na wengine pia tupate fursa zaidi. Pia tutaenda kutoa elimu tuliyoipata kwa vikundi ambavyo havikupata mikopo awamu hii,” alisema Nombo.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3